Tshabalala apewa mkataba wa kishua

BEKI Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ametambulishwa usiku wa juzi akiwa mmoja ya nyota wapya wa Yanga akitokea Simba, lakini saini ya mkataba uliomfanya avae uzi wa Jangwani si mchezo kutokana na mkwanja aliovuna kutoka kwa mabingwa hao wa soka wa Tanzania.

Tshabalala ambaye Mwanaspoti liliripoti juu ya dili lake kutua Jangwani baada ya kumaliza mkataba Simba na kushindwa kuafikiana na mabosi wa Msimbazi, linafahamu kuwa katika mkataba wa miaka miwili atavuna zaidi ya Sh600 milioni likiwa ni dau la usajili.

Dau hilo liliifanya Simba kurudi nyuma kukubali kuzidiwa na Yanga na kumuachia nahodha huyo aliyetumikia timu hiyo kwa miaka 11 tangu 2014 alipotokea Kagera Sugar.

Beki huyo wa kushoto inadaiwa atakuwa anapewa mshahara mkubwa wa Sh25 milioni kwa mwezi ambapo kwa miezi 24 aliyosaini atachukua kiasi cha Sh600 milioni.

Ukichukua mishahara huo na lile dau la usajili Tshabalala atakunja kiasi cha sh 1.2 Bilioni akiwa ndani ya Yanga.

Tshabalala pia atapewa gari yenye thamani ya Sh30 milioni, lakini atalipiwa nyumba ya gharama ndani ya klabu hiyo.

Beki huyo pia akihusika kutengeneza kwa kutoa asisti mabao kuanzia 10 kuna kiasi ambacho atavuna huku akipewa dili la matangazo mbalimbali ya tajiri wa Yanga Ghalib Said Mohammed ‘GSM’.

Ndani ya Yanga beki huyo sasa atakuwa anakimbizana na mabeki wenzake Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambao wanavuna kiasi kama hicho. Yanga bado haijamtambulisha Tshabalaa ikisubiri amalize majukumu ya timu ya taifa ambapo mabosi wa klabu hiyo wanataka kufanya mambo mazito kwenye utambulisho wake kulipa kisasi cha walichofanyiwa kwenye utambulisho wa mshambuliaji Mghana Jonathan Sowah wakati anatambulishwa na wekundu hao.

“Kuna mambo tunayapanga tunataka awe mchezaji wa mwisho kumtambulisha. Wanayanga watafurahi lakini kuna wengine wa nje watanuna sana kwenye huu utambulisho,” alisema bosi huyo wa juu.