Uagizaji wa gesi ya kupikia kwa pamoja mbioni

Dar es Salaam. Serikali iko mbioni kuja na mpango wa uagizaji wa gesi ya kupikia kwa pamoja kupitia Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) baada ya miundombinu wezeshi kukamilika kujengwa.

Mfumo huo unatajwa kusaidia kupunguza bei ya gesi ya kupikia jambo litakalowawezesha wananchi kumudu gharama yake na kuachana na matumizi ya nishati safi.

Hayo yamesemwa wakati akiwasilisha mafanikio ya ofisi yake katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioratibiwa na ofisi ya Msajili wa Hazina uliofanyika leo Agosti 7, 2025.

Uamuzi huo unakuja wakati ambao uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeleta matokeo chanya ikiwamo kuongeza kiwango cha mafuta kinachopokewa nchini, kuvutia nchi jirani kuagiza mafuta kupitia Tanzania na kuokoa kiwango cha mafuta kilichokuwa kikipotea awali.


Mtendaji Mku wa PBPA, Erasto Simon alizitaja sababu za gesi ya kupikia kutoagizwa kwa kutumia mfumo wa pamoja kuwa ni miundombinu iliyopo inaruhusu meli ndogo pekee kuingia.

“Hivyo, unapoingia mfumo kama huu unalazimika kukusanya mahitaji makubwa ili kuweza kuagiza mzigo mkubwa, hivyo kinachofanyika sasa ni kujenga miundombinu ya meli kushusha mizigo na hifadhi kubwa na hayo yatakapokamilika gesi ya kupikia itaingizwa katika mfumo wa wakala wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja,” amesema.

Akielezea baadhi ya kazi zinazofanyika amesema ni kujenga miundombinu ya ushushaji gesi ya kupikia, kujenga sehemu ambazo meli kubwa zitakaa, kutanua mabomba ili yaweze kusukuma mzigo mkubwa kwenda kwenye maghala.

“Miongoni mwa faida za kuagiza mzigo wa gesi ya kupikia kwa pamoja maana yake bei itakuwa ya chini kwani gharama itapungua na wananchi wataweza kunufaika,” amesema.


Akizungumzia suala hili, Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma wa Mafuta na Gesi Tanzania, Abdulsamad Abdulrahim amesema mpango huo ni mzuri hasa kama Serikali itajikita zaidi katika kujenga miundombinu na kutoingia katika biashara moja kwa moja.

Hiyo, itatoa fursa kwa watu waliowekeza ikiwamo raia wa kigeni kuwa na uhakika wa kile wanachokifanya badala ya kuwa katika ushindani na Serikali.

“Itasaidia kwa kiasi kikubwa katika mhamo kuelekea nishati safi na kuachana na matumizi ya mkaa ambao unaleta athari kwa binadamu. Hivyo, miundombinu kama hii inapowekwa ni vyema Serikali iangalie wawekezaji waliopo na kuwawekeza mazingira mazuri,” amesema.

Hili linakwenda kufanyika wakati ambao uagizaji wa mafuta kwa pamoja umevutia idadi ya kampuni zinazoshiriki kwenye mchakato wa uagizaji mafuta zimeongezeka kutoka 33 Mwaka 2021 hadi 73 Mwaka 2025.

Hilo limechochea kuongeza kiwango cha uagizaji mafuta nchini kupitia mfumo huo kutoka wastani wa tani 5,805,193 mwaka 2021 hadi tani 6,365,986 mwaka 2024 huku zikitarajiwa kufikia Tani 7,090,165  Desemba 2025.

“PBPA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania imeendelea kupanga ratiba za meli za kuleta mafuta nchini ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya bandari zetu na kupunguza gharama za meli kusubiri,” amesema Simon.

Amesema hatua hiyo imesaidia kuokoa Sh29.95 bilioni kwa mwaka zilizokuwa zinatumika huku taarifa za taarifa za mafuta yanayoingia nchini kupitia mfumo huo zikitunzwa kikamilifu.

Kutokana na kujua kiwango cha mafuta kinachohitajika, kulisaidia kuongeza uwekezaji katika maghala ya kuhifadhi mafuta 22 mwaka 2021 hadi 24 mwaka 2025, huku uwezo wa kuhifadhi ukiongezeka kutoka lita bilioni 1.288 hadi lita bilioni 1.72.

“Jambo hili limeweka uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini kwani tumekuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kidunia kama vile Uviko-19 na vita baina ya Urusi na Ukraine na vita baina Iran na Israel.

Katika kipindi chote nchi imekuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji, wakati wote pamoja na kuhudumia nchi jirani,’ amesema.

Kufungwa kwa mifumo ya kutambua kiwango halisi cha mafuta yanayopokewa kwenye hifadhi za mafuta kutoka melini nalo ni jambo ambalo limefanyika hali iliyoongeza udhibiti wa udanyanyifu katika kiasi cha mafuta yanayopokewa kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta.