Ninahuzunishwa na kusikitishwa sana na kile kinachoendelea katika mitandao ya Kijamii hapa Tanzania kwa baadhi ya Watanzania kufurahia madhila yanayowapata wenzetu ikiwamo kifo, jambo ambalo tunapaswa kulitafakari kama taifa.
Haya yanayoendelea mitandaoni siyo ya kupuuza hata kidogo kwa sababu huko ndiko mijadala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi imehamia na tusisahau kuwa huko ndiko Watanzania walio wengi hasa vijana wapo huko.
Ripoti ya Takwimu ya Sekta ya Mawasiliano ya Robo mwaka inayoishia Juni 2025 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaonyesha hadi kufikia Juni 2025, Tanzania ilikuwa na watumiaji wa Intaneti milioni 54.1.
Sasa katika hao, idadi ya laini zinazotumia huduma ya Intaneti ni milioni 48.0 na hizi ndio baadhi zinaingia kwenye Facebook, Instagram, Tovuti mbalimbali, mtandao wa X (zamani Twitter), X Space na Club House ambako mijadala ipo.
Nimebahatika kuingia katika mijadala mbalimbali katika X Space au Twitter Space na Club House ambako unakuta washiriki ni kati ya 600 hadi zaidi ya 1,000 na mjadala ukiwa una hisia na unagusa watu wengi, washiriki wanafika hadi 10,000.
Ninaamini na nadhani hata wewe, utakubaliana na mimi kuwa kwenye mitandao ndiko ambako sasa kunatumika zaidi kufikisha ujumbe kwa sababu ujumbe unaotumwa unamfikia moja kwa moja mlengwa na asiyemlengwa wa ujumbe.
Ukitaka kujua kiwango cha chuki cha Watanzania walio wengi katika mitandao ya kijamii, nenda katika ukurasa wa kiongozi wa Serikali, CCM au vyombo vya habari vilivyotuma taarifa za vifo au ajali za viongozi halafu soma maoni ya wachangiaji.
Ukweli una sifa moja tu, kwamba hata ukiukataa namna gani huwa haugeuki kuwa uongo, ni lazima kwanza kama taifa tukiri hatupo tena wamoja, chuki miongoni mwetu imetamalaki na hisia za visasi zinatutafuna. Kwanini tumefika hapa?
Ni lazima kuna mahali tumejikwaa na ni vyema tukatafuta nini kilisababisha tukajikwaa na siyo kuangalia pale tulipoangukia, kwa sababu chuki zinazoenezwa mitandaoni zina athari kubwa kwa upendo, amani na mshikamano wetu.
Sasa hivi ni jambo la kawaida na linalotaka kuzoeleka katika huko katika Jamhuri ya X (zamani Twitter), Facebook, Instagram na Whatsapp kwamba kunapotolewa tangazo la kifo cha kiongozi wa Serikali au polisi baadhi ya watu wanashangilia.
Siyo kushangilia tu, lakini kama ni ajali na wapo walionusurika, watu hao wanaenda mbali na kuwaombea mabaya zaidi yawakute na ndio maana najiuliza nini kimesababisha baadhi yetu kukosa utu na upendo, ulioasisiwa na waasisi wetu.
Hali kama hii tunayoina hapa Tanzania leo, tuliishuhudia Aprili 6,1994 wakati wa Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana na Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira walipokufa katika ajali ya pamoja ya ndege wakitua uwanja wa ndege wa Kigali.
Baadhi ya wakimbizi waliokuwa katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma, walifurahia kutunguliwa kwa ndege ya marais hao na wakafanya sherehe kuwa maadui zao wakubwa waliowapa mateso wanayopitia walikuwa wamekufa.
Takribani miaka 30 imepita, hali hii inaanza kujitokeza nchini Tanzania katika mazingira tofauti kwani wakati ule sumu ya visasi ilisambazwa baina ya mtu na mtu, lakini sasa inasambazwa katika mazingira ya kukua kwa teknolojia.
Ndani ya sekunde moja, taarifa iliyowekwa mitandao niliyoitaja kutoka Songea, inaweza kumfikia mtu aliyepo Kigoma na kwa maneno mengine upashanaji habari hauwezi kudhibitiwa tena, ziwe ni nzuri au habari hasi dhidi ya watawala.
Mathalan, taarifa za kifo cha aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la 11 na Bunge la 12 mwanzoni mwanzoni, Job Ndugai zilisambaa saa chache kabla ya taarifa rasmi kutolewa na Bunge, ni ilisambaa Kusini hadi Kaskazini, Mashariki hadi Magharibi.
Hata hivyo, kinachonihuzunisha, ni kusambaa kwa video ya kikundi cha watu wanaosemekana ni kutoka moja ya kata ya jimbo lake la Kongwa, wakiandamana usiku wakishangilia kifo chake, ninajiuliza, hivi Watanzania tumefikia huko?
Inawezekana tukasema hawa ni wale ambao wamechukizwa na matokeo ya kura ya maoni ndani ya CCM zilizofanyika Agosti 4, 2025, lakini na hao walioko mitandaoni nao Job Ndugai aliwakosea nini? Kuna mahali tumeteleza kama taifa.
Leo Agosti 7, 2025 nimeona mitandaoni, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Simon Mayeka akisikitishwa na video ya baadhi ya wananchi wa Kongwa wakishangilia kifo cha Ndugai akisema si utamaduni wa Watanzania kushangilia mauti.
Ni kweli siyo utamaduni wa Watanzania kufurahia vifo vya viongozi wetu au hata mtu yeyote yule, hilo nami linaniumiza sana, lakini swali tunalopaswa kujiuliza nini kimetufikisha hapo? Kuna mahali viongozi wetu wamewakosea Watanzania hawa?
Mbona ninaona hawa siyo wale Watanzania ninaowafahamu ambao hata kama ni mtu ulikuwa ukimchukia kiasi gani, anapokuwa amekufa, tunatanguliza utu mbele na mabaya yake yanawekwa kando na watu wanaungana kuomboleza na wafiwa.
Kuna ambao watasema inawezekana ni tofauti za kiitikadi zilizoletwa na vyama vya siasa ndio imetufikisha hapo, lakini tusisahahu wako ambao wanaoombea vifo baadhi ya viongozi wetu, Polisi wetu na viongozi wa CCM ambao ni watu huru.
Ni lazima sisi kama Watanzania tutafakari nini kinalitafuna taifa letu nini kimetufikisha hapa lakini ninachokidhani mimi kimetufikisha hapa ni kwamba kuna kundi la Watanzania wanaona haki inakandamizwa si uraiani, si mahakamani.
Lipo kundi linaona kama vyombo vyetu vya dola hasa Polisi, hawajatekeleza ipasavyo katika suala zima la utekaji wa watu, kupotea kwa watu, mauaji, kuumizwa na kujeruhiwa kwa watu na hawaridhiswi na hatua za upelelezi.
Kauli za mizaha na zisizotia matumaini kwa ndugu, jamaa na marafiki ambao wanawalilia wapendwa wao ambao hawaonekani hadi leo wengine zaidi ya miaka 7 na wengine wiki mbili sasa, zimezalisha chuki zinazowatafuna watawala.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na Uchaguzi Mkuu 2020 umezalisha chuki na majeraha ya kisiasa, ambayo tiba pekee ni maridhiano ya kisiasa kama kweli tunaitakia mema nchi hii na tutumie 4R za Rais Samia kufika huko.
Baba wa Taifa, hayati Jullius Nyerere aliwahi kusema “Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo”, nami naomba niazime usemi huo kuwa tusijidanganye nchi iko salama, kuna kitu kinafukuta chini kwa chini.
Kuna jambo ambalo haliko sawa, tulitafute na kama kuna jambo watawala wanajua limetufikisha hapa, basi walirekebishe mapema wakati wa uhai wao kwa sababu, kwa waamini wa Kikristo tunaamini kuna moto kwa waliotenda mabaya.
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema maisha ya mwanadamu hapa duniani ni hadithi tu, sisi wenyewe ndio tutaamua wale watakaosimuliwa hadithi zetu, wasimuliwe hadithi nzuri au mbaya.
Ninatamani Serikali hata kwa kutumia mitandao ya Survey Monkey au Google Form, watafute maoni kwa Watanzania ya nini kimesababisha chuki hizi tunazozishuhudia na tufanyeje kulirudisha taifa letu katika umoja na mshikamano.
Haifurahishi hata kidogo kuna ni jambo linataka kuzoeleka kwamba baadhi ya viongozi wakitangulia mbele ya haki au wabunge wa CCM na Polisi wetu wakidhurika tunashangilia, hili ni taifa lingine kabisa siyo lile lilioachwa na Nyerere.
Sote tunakumbuka tukio la Kibiti mkoani Pwani ambako wapiganaji wetu wapatao nane kutoka Jeshi la Polisi waliviziwa (ambushed) na kushambuliwa kwa risasi na wote walifia pale pale, wapo watu waliokosa utu walishangilia mitandaoni.
Tutafute tulipojikwaa, tusiangalie tulipoangukia. Huo ndio ushauri wangu kwa sababu wasawahili wanasema kunapofuka Moshi, chini huwa kuna moto.