Uhondo wa CHAN upo Nairobi

UHONDO wa fainali za CHAN 2024 unaendelea leo kwa mechi mbili za Kundi A, mapema jioni DR Congo itavaana na Zambia kabla ya wenyeji Kenya kumalizana na Angola, mechi zote zikipigwa jijini Nairobi.

Saa 10:00 jioni, DR Congo iliyoanza michuano hiyo kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji Kenya, itavaana na Zambia inayotupa karata ya awali ya fainali hizo za nane kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, kabla ya saa 1:00 usiku Harambee Stars itakwaruzana na Angola iliyochezea kichapo cha 2-0 kutoka kwa mabingwa mara mbili Morocco kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani.

Mechi hizo zinatarajiwa kuwa zenye ushindani kutokana na matokeo waliyopata mabingwa wa kwanza wa fainali hizo DR Congo na Angola moja ya timu zinazopigiwa chapuo kupenya hatua ya makundi kwenda robo fainali kutoka katika kundi hilo.

Zambia ambayo inatupa karata ya kwanza itakuwa na kazi ya kuhimili hasira za DR Congo iliyolala mbele ya Kenya katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa wikiendi iliyopita, lakini Angola ikitesti zali kwa wenyeji ili kuepuka kuingia katika hatari ya kuwa timu ya kwanza kuaga michuano hiyo katika kundi hilo la kifo.

Hii ni mara ya pili kwa Zambia na DR Congo kukutana katika CHAN, ambapo mwaka 2009 zilikutana nusu fainali na Wakongomani kushinda kwa mabao 2-1 na kutinga fainali kabla ya kubeba ubingwa kwa kuifunga Ghana kwa mabao 2-0.

Lakini zimeshakutana mara kadhaa katika mechi za Afcon na zile za mchujo wa Kombe la Dunia tangu 1973, huku rekodi zikionyesha DR Congo imekuwa mbabe mbele ya Zambia kwani katika mechi 11 za mashindano yote Zambia imeshinda mara moja tu na kupoteza tano mbele ya wenzao na mechi zilizobaki ziliisha kwa sare.

Zambia imeitambia DR Congo katika mechi mbili za kirafiki ilizowahi kukutana hivi karibuni na mechi za mwisho za michuano ya Afrika timu hizo zilitoka sare ya 1-1 mapema mwaka jana zilipokuwa kundi moja la Afcon zilizofanyika Ivory Coast sambamba na Tanzania.

Kwa upande wa Kenya dhidi ya Angola zilikuwa katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Afcon 2012 na kila moja ilishinda nyumbani, Kenya ilianza kwa ushindi wa 2-1 kabla ya Angola kupindua meza na kusonga mbele kwa bao la ugenini kwa kushinda 1-0.

Hivyo kwa mechi za CHAN ni mara ya kwanza kukutana na kila moja ikiwa na kiu ya ushindi, Angola kutaka kujiweka pazuri katika kundi hilo lakini Kenya kuendeleza ubabe kama wenyeji, huku kocha Benny McCarthy akiwa na kazi kubwa ya kuizuia Angola inayosifika kwa kucheza kwa kasi.