Ukosefu wa elimu chanzo changamoto za afya ya uzazi

Unguja. Mojawapo ya sababu inayochangia vijana kuwa na changamoto kuhusu afya ya uzazi na hedhi salama ni ukosefu wa elimu, imeelezwa.

Kutokana na hilo, jamii imesisitizwa kutoa elimu ya masuala hayo kwa vijana ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kwa kufanya hivyo imeelezwa afya bora itaendelezwa ili kusaidia kuleta uelewa mpana kwao na kupanga familia za matarajio yao.

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, Amour Yussuf Mmanga amesema hayo leo Agosti 7, 2025 alipofunga bonanza la michezo lililoandaliwa na Baraza la Vijana Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi ya Michezo kwa Maendeleo (Mima).

Amesema lengo la bonanza hilo ni kuleta uelewa kwa jamii hasa vijana kutambua elimu ya afya ya uzazi jambo litakalosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Vilevile kusaidia vijana kupanga familia zao katika hali nzuri na salama.

“Vijana wengi hukutwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya uzazi na hedhi salama hali inayotokana na ukosefu wa elimu hiyo,” amesema.

Amesisitiza, Taifa linahitaji kuwa na maendeleo endelevu, hatua itakayofikiwa kwa wananchi kuwa na afya bora na imara.

Pia, amewataka vijana kuzitumia fursa zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiwamo mikopo ili kujiajiri na kujikimu kimaisha.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan amewataka vijana kutumia elimu waliyoipata na kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa jamii, kwani vijana ndio kundi linalokumbwa na changamoto za kiafya.

Wakati huohuo, Wizara ya Afya Zanzibar imepokea ugeni kutoka Shirika la kimataifa la The Neighbourhood Organization and Humanity (Nohfi) la nchini Canada, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya, hasa maeneo ya afya ya mama na mtoto pamoja na watoto wenye maradhi ya moyo.

Akizungumza baada ya kupokea ugeni huo ofisini kwake Vuga, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema ziara hiyo inalenga kufanya tathmini ya hali ya utoaji wa huduma za afya katika vituo mbalimbali na hospitali zilizopo Unguja na Pemba.

“Lengo ni kujionea changamoto zilizopo katika utekelezaji wa huduma za afya ili kwa pamoja tuweze kuzitatua na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma bora kwenye afya ya msingi,” amesema.

Amesema shirika hilo limeonyesha dhamira njema ya kusaidia sekta ya afya na limetoa msaada wa zaidi ya Dola milioni 30 za Marekani (zaidi ya Sh78 bilioni) katika nchi mbalimbali duniani, hivyo ujio huo kwa Zanzibar ni fursa muhimu ya kushughulikia changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa huduma bora kwa mama na mtoto na watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nohfi, Mohammad Firaaz Azeez amesema shirika hilo linapanga kuimarisha programu za utunzaji wa afya ya moyo wa watoto na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa wajawazito kuanzia ngazi ya jamii hadi vituo vya afya.

“Tunataka kuona kila mama na kila mtoto anapata huduma za afya zinazostahiki kwa wakati, ushirikiano huu utaweka mkazo katika kuimarisha huduma za msingi,” amesema.

Mshauri mkuu wa kidiplomasia wa Nohfi, Balozi Ebrahim Rasool amesisitiza kuwa, shirika hilo limejipanga kuimarisha huduma za afya barani Afrika kwa kushirikiana na Serikali, mashirika ya kijamii na wadau wa kimataifa ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia watu wote hususan waliopo katika maeneo hatarishi.