Unguja. Katibu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Zena Ahmed Said amewataka vijana wanaopata nafasi za mafunzo yanayotolewa na Serikali kuzitumia vizuri ili kuongeza ubunifu.
Amesema hayo leo Alhamisi Agosti 7, 2025 alipofungua mafunzo ya upambaji wa uso katika mradi wa kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika unaosimamiwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea).
Zena amesema wapo baadhi ya watu ambao wakipata fursa za aina hiyo huzibeza na kusahau kuwa kuna wengine wanazililia na hawazipati.
Kutokana na hilo, amewataka waliopata fursa ya kuchaguliwa kushiriki mafunzo hayo wazitumie vizuri.
Pia ametoa agizo kwa wakala huo kwamba, mwanafunzi ambaye hatakuwa na mahudhurio mazuri katika mafunzo hayo pasipo kuwa na sababu ya msingi wamwondoe na watafute mwingine.

Wanafunzi wa waliopata nafasi ya Mafunzo ya upambaji wa uso yanayosimamiwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar.
“Akitokea mwanafunzi mtoro na anatoa sababu zisizoeleweka lazima mumtoe ili aingie mwingine anayeweza kuitumia fursa hiyo ipasavyo, kwani mafunzo hayo hayawagharimu chochote,” amesema.
Zena amewashauri wakufunzi kutoa mafunzo ya upambaji wa aina mbalimbali na isiwe ya kumfanya mtu kuwa mrembo pekee, badala yake wafunzwe aina nyingine ikiwamo upambaji wa filamu za kutisha kwa lengo la kuendana na soko la ajira.
Amewataka wanafunzi baada ya kumaliza mafunzo hayo kuitumia mitandao ya kijamii kutangaza kazi zao ili kuvutia wateja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zeea, Juma Burhan Mohamed amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa wanafunzi 200 na kwa awamu ya kwanza wataanza na 50 na yatadumu kwa mwezi mmoja.
Amesema mafunzo hayo yatatolewa Unguja na Pemba na mbali ya upambaji, wanafunzi watafundishwa kuhusu utunzaji fedha, ukuzaji wa biashara na upatikanaji wa masoko.
Meneja mradi, Salum Mkubwa Omar amesema unasimamiwa na Wizara ya Elimu Zanzibar ili kuwajenga vijana kuwa na sifa za kuajirika na kuajiriwa.
Mkufunzi msaidizi wa mafunzo hayo, Radhia Abdalla Bakari amesema vijana wanapaswa kuzingatia masuala ya urembo na waache tabia ya kuwatolea wateja maneno yasiofaa, kwani hilo linaharibu soko la biashara hiyo.
Mwanafunzi, Hawa Jumanne ameshukuru kwa kupata nafasi ya mafunzo akiahidi kuyatumia vyema ili kuboresha kazi yake anayoamini itamuingizia kipato.