Dar es Salaam. Walimu wa shule za awali na maofisa elimu ngazi ya kata wamepewa mafunzo ya kutambua viashiria vya awali vya usonji kwa watoto.
Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam yamelenga kuwapa walimu uelewa wa kutambua tofauti za tabia na mawasiliano kwa watoto wenye Usonji, ikiwa ni pamoja na kutocheka, kutokujibu wanapoitwa, kurudia matendo yale yale mara nyingi, au kuepuka kuangalia mtu usoni.
Malengo mengine ni kuwawezesha walimu kupata maarifa na mbinu za awali za kutambua dalili za Usonji kwa watoto, na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwashauri wazazi kuwapeleka watoto kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi na huduma za kitaalamu.
Akizungumza leo Agosti 7, 2025 katika mafunzo hayo, daktari bingwa wa watoto katika mfumo wa fahamu na ubongo, Edward Kija amesema walimu wa awali ni kiungo muhimu katika mnyororo wa utambuzi wa changamoto za ukuaji kwa watoto wadogo.
“Walimu hawa ndio wanaokuwa na watoto kwa muda mrefu nje ya familia hivyo kuwajengea uwezo wa kutambua viashiria vya usonji ni hatua muhimu katika kuhakikisha watoto wanagunduliwa mapema na kusaidiwa kwa wakati,” amesema Dk Kija.
Kwa upande wa mwalimu wa shule ya awali ya Kijitonyama, Rehema Musa amesema elimu waliyoipata imewapa mwanga mpya kuhusu namna ya kutambua tofauti za kitabia kwa watoto na umuhimu wa kutoa msaada mapema.
“Tumezoea kudhani kuwa mtoto anayekaa kimya au asiyependa kucheza na wenzake ni mgumu kuelewa. Lakini sasa tunajua huenda ni viashiria vya Usonji mafunzo haya yamebadili kabisa mtazamo wetu,”amesema mwalimu Musa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Lukiza Autism Foundation (LuAF), Hilda Nkabe amesema wanatarajia kufikia shule 100 na walimu zaidi ya 300.
Amesema hatua hiyo itasaidia kugundua takribani watoto 25 wenye viashiria vya usonji kwa mwaka mmoja, ikizingatiwa takwimu za kimataifa zinazoonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya kila 100 anaweza kuwa na hali hiyo.
“Tunataka kila mtoto apate nafasi ya kujifunza na kustawi ili hilo lifanikiwe, jamii nzima ikiwemo walimu, wazazi na wataalamu wa afya, wanapaswa kushirikiana. Mradi huu ni sehemu ya dira yetu ya kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma,” amesema Nkabe.
Amesema mradi huo unaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hasa eneo la maisha bora na ustawi kwa wote, huku akiitaka jamii na mashirika mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa rasilimali na msaada wa kitaalamu.