Wanaoficha watoto wenye mahitaji maalumu kusakwa

Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya imesema inaanza msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini na kuwachukulia hatua wazazi na walezi wanaoficha watoto wenye mahitaji maalumu.

Pia, imewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu katika malezi na inapotokea kutoelewana kwa wanandoa katika familia kutoathiri maisha ya mtoto, hasa katika haki yake ya elimu.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 7, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi wa Tuwawezeshe wafikie ndoto zao kupitia Shirika la Twende Wote Foundation, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema wataanza msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini wanaoficha watoto hao.

Mbali na hilo, amesema suala la watoto kuzagaa mitaani jijini humo halina afya kwani Serikali inatoa elimu pasipo malipo kwa shule za msingi na sekondari.

“Tumeshaanza na tunaendelea na msako wa nyumba kwa nyumba, lazima tuchukue hatua kali kwa wazazi na walezi wanaoficha watoto wenye uhitaji maalumu na kutopewa huduma,” amesema na kuongeza:

“Kila mzazi atimize wajibu wake kwenye familia, tusiruhusu ndoa kuvunjika, hata kama mapenzi yanaisha lakini tuwalee watoto kwa kuwapeleka shule wapate elimu, tukifanya hivi tutaondoa watoto mtaani.”

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Tuwawezeshe wafikie malengo, hafla iliyofanyika leo Agosti 7 Kata ya Iwambi jijini Mbeya



Itunda amesema halmashauri hiyo imetoa zaidi ya Sh3.2 bilioni za mikopo kupitia asilimia 10 mapato yake kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa mradi huo, Devule Mwambije amesema umeanzishwa baada ya utafiti walioufanya katika kata 36 za Jiji la Mbeya kubaini wimbi la wazee, wanawake, watoto na wenye ulemavu kuhitaji msaada.

Amesema wakati wa jioni kundi kubwa la watoto hujikusanya hususani eneo la Kabwe kuomba msaada kutokana na changamoto zinazowakabili.

Kupitia mradi huo, amesema wameanza na watoto 36 katika Kata ya Iwambi. Mkakati uliopo amesema ni wa kutoa huduma nje ya Mkoa wa Mbeya.

“Tuliona wengi wanaomba msaada, tukatathimini wanaowasaidia kuna muda watakata tamaa au kuishiwa je, wataishije? Tukaamua kuja na mradi huu ambao utawafikia moja kwa moja na hatuishii Kata ya Iwambi bali tutasambaa nje ya mkoa,” amesema.

Mwambije amesema kwa kuanzia, watoto hao watapewa elimu kwamba, mwakani watakaofaulu watawapa kadi za bima za afya na kusimamia masomo yao ya sekondari. Amewaomba wadau kushirikiana kutokomeza watoto mitaani.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iwambi, Lugano Mwamsojo amesema mradi huo unaweza kuwa mwarobaini katika kuzuia makundi ya kihalifu katika mitaa na kuwaomba wananchi kuunga mkono shughuli za wadau na Serikali.

“Tuwaunge mkono wadau wanaowafikia watoto wetu kwa misaada, Serikali inajitahidi kuwapa huduma wananchi, hivyo niwaombe tuendeleze ushirikiano, amani na utulivu kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema.