World Vegetable Centre ‘yajitoa kubireshs kilimo cha mbogamboga

…,…………..

Kituo cha Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo  cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini Mwa Afrika (World Vegetable Center) kilichopo Tengeru, Arusha, kimesema kuwa kitaendelea kuongeza juhudi za kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo hapa nchini na Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia tafiti za kisayansi, ukuzaji wa mbegu bora na uwekezaji katika rasilimali watu

Kituo hicho kimeweka kipaumbele katika kuzalisha mbegu chotara bora zinazohimili ukame na magonjwa, zikiwamo mboga muhimu kama nyanya, vitunguu, pilipili, kabichi pamoja na mboga za asili zenye virutubisho vya hali ya juu.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya uzalishaji wa mbegu bora kwa mazao yanayohimili magonjwa na ukame yaliyofanyika hivi karibuni katika kituo hicho mkoani Arusha, Dk Sognigbe N’Danikou, mtaalamu wa utunzaji na matumizi ya mbogamboga asilia kutoka kituo hicho amesema lengo ni kukuza kizazi kipya cha wataalamu watakaoongoza sekta hiyo kwa kutumia maarifa ya kisayansi.

“Tunajikita katika kufanya tafiti na kuzalisha mbegu bora za chotara zinazoweza kustahimili hali ngumu ya hewa na mashambulizi ya magonjwa, lakini muhimu zaidi ni kuandaa wataalamu wakiwemo wa ndani wenye uwezo wa kusaidia wakulima moja kwa moja,” amesema Dk N’Danikou.

Mbali na tafiti na mafunzo, kituo hicho pia hufanya kazi ya moja kwa moja na wakulima wadogo kuwapatia mbegu bora pamoja na mafunzo ya mbinu bora za kilimo, lengo likiwa ni kuongeza mavuno, kuboresha usalama wa chakula na lishe hasa katika jamii zenye kipato cha chini.

Mmoja wa wanaohudhuria mafunzo hayo, Daktari Aloyce Callist Kundy kutoka Benki ya Vinasaba vya Mimea iliyo chini ya Mamlaka ya Viuatilifu na Mimea (TPHPA) amesema Tanzania imekua na mahusiano mazuri na Taiwan katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kwa kufanya tafiti zenye kukuza sekta hiyo hapa nchini.

Naye Magdalena Kiungo, mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela anayesomea uzalishaji wa mbegu bora za kisasa amesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo, hasa katika uzalishaji wa mbegu bora zenye kutoa mazao mengi na kuhimili ukame.