CUF yafuta saba uanachama kwa kuzipiga mkutanoni

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimewafuta uanachama makada saba wanaodaiwa kuwashushia kichapo wajumbe wenzao wa Baraza Kuu la chama hicho.

Hata hivyo, baadhi ya waliotimuliwa wamepinga hatua hiyo wakisema hawajapewa fursa ya kusikilizwa, hivyo inakiuka misingi, katiba na taratibu za chama hicho.

Waliofutwa uanachama na Baraza Kuu la chama hicho ni Dauda Hassan, Yassin Ngotwa, Abdallah Dugwa, Faki Mohamed, Rashid Hamad, Mohammed Nassoro na Yusuph Mussa.

Kosa lao limetajwa kuwa ni kuleta vurugu kwenye kikao kilichofanyika Agosti 6, 2025 katika ukumbi wa Shaban Mloo, makao makuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda ya kupitisha ilani ya chama hicho na kupitia majina ya wagombea wa urais wa Tanzania na Zanzibar, watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.

Kutokana na vurugu hizo, kikao kililazimika kusimama kwa muda.

Chanzo cha vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya wajumbe kupata majeraha kiasi cha kwenda hospitali kutibiwa, ni kitendo cha kutaka walioingia kwenye kikao hicho ambao si wajumbe halali watolewe nje kupisha shughuli iliyowakusanya ifanyike.

Jambo hilo halikutekelezwa kwa kinachoelezwa na viongozi kuwa walengwa hao walikuwa wageni, lakini ni wajumbe halali, hivyo ni lazima washiriki.

Uamuzi huo ulizua vurugu ndani ya ukumbi, huku baadhi wakikosa upenyo wa kutokea baada ya madirisha na milango kufungwa.

Baada ya vurugu kutulia, kikao hicho cha kikao hicho cha siku mbili kiliendelea, lakini wajumbe 25, wakiwemo hao saba waliofutwa uanachama, walisusia kushiriki na kurudi Zanzibar.

Akizungumza hatua iliyochukuliwa na Baraza Kuu la chama hicho, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema wajumbe hao kabla ya kuanzisha vurugu waligoma kusaini karatasi ya mahudhurio ya kikao wala kutoka ndani ya ukumbi.

“Tuliwataka watoke ili kikao kiendelee kwa amani waligoma kwa sababu wajumbe waliowakataa walikuwa wageni, tuliwasihi lakini waligoma na kuzidisha vurugu kiasi cha kupelekea viongozi wa chama kutoka kwenye ukumbi,” amesema Profesa Lipumba.

Amesema wajumbe hao walikuwa na lengo baya la kutaka kukwamisha kikao hicho kwani hata walipotulizwa waliendelea kuleta vurugu bila kujali umuhimu wa jambo lililokuwa limewapeleka.

“Baraza Kuu kwa kuzingatia mamlaka lililopewa kikatiba yanayopatikana ibara ya 83, ya chama chetu ya mwaka 1992 toleo la 2015 lilijadili makosa ya utovu wa nidhamu yaliyofanywa hadharani na baadhi wajumbe kwenye kikao cha Agosti 6, 2025,” amesema na kuongeza:

“Baraza kuu limekubaliana vinara wa vurugu na utovu wa nidhamu uliofanywa hadharani na wamekuwa na rekodi ya kufanya vurugu ndani ya chama kwa muda mrefu, wafutwe uanachama.”

Moja wao, Rashid Hamad akizungumza na Mwananchi amesema taarifa hizo walishazipata tangu jana (Agosti 7), lakini hatua hiyo ni batili kwani hawajaitwa kusikilizwa kujua sababu iliyofanya kuanzisha vurugu.

“Katiba yetu imeeleza bayana mtu hawezi kuthibitika ametenda kosa bila kuitwa kusikilizwa, lakini wao wamejikusanya na kuchukua hatua hiyo. Tunasema ni batili, kwanza inakiuka misingi ya katiba na taratibu za chama chetu,” amesema.

Amesema hoja kuhusu wajumbe wasio halali kwenye kikao ilikuwa sahihi na ya msingi, lakini viongozi wa chama hicho hawakuipenda, badala yake waliwakingia kifua.

Mohamed Nassoro naye  amesema hawakubaliana na uamuzi huo kwa kuwa hawajaitwa, pia hawajapewa barua rasmi kuhusu uamuzi huo.

“Tunasubiria tuletewe taarifa rasmi tutajua uamuzi wa kuchukua, lakini ninachoweza kusema kwa sasa, uamuzi huo ni batili, hatujapewa nafasi ya kusikilizwa,” amesema.