Arusha. Mahakama ya Rufaa imefuta adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela aliyohukumiwa mkazi wa Longido mkoani Arusha, Loy Lesila, aliyetiwa hatiani kwa kosa la ubakaji.
Uamuzi wa mahakama umefikiwa baada ya kubaini kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka.
Jopo la majaji Rehema Mkuye, Lucia Kairo na Gerson Mdemu lililoketi Arusha lilitoa hukumu hiyo Agosti 5, 2025 na nakala kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Majaji baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, lilibaini kuwapo dosari za kisheria, ikiwamo utambuzi wa mrufani eneo la tukio.
Jaji Mdemu aliyeandika hukumu hiyo kwa niaba ya jopo amesema kabla ya kupokewa ushahidi wa upande wa mashtaka katika mahakama ya chini, rekodi ya rufaa inaonyesha kulikuwa na dalili za kutumika mkalimani katika kesi hiyo na kabla shahidi wa kwanza kuanza kutoa ushahidi ilielezwa mahakamani kuna mkalimani.
Amesema mkalimani hakufichuliwa na rekodi iko kimya hadi mwisho wa kesi, ikiwa huduma ya mkalimani huyo asiyejulikana iliwahi kutumika, hivyo ina maana kama alivyowasilisha wakili wa Jamhuri mashahidi wote walitoa ushahidi bila ushahidi wao kutafsiriwa.
Mahakama ya Wilaya Longido ilimtia hatiani na kumhukumu mshtakiwa (mrufani) kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka msichana wa miaka 16.
Upande wa mashtaka ulidai kosa hilo lilitokea Novemba 15, 2019 katika Kijiji cha Orkejuloongishu-Ketumbeine, wilayani Longido, Mkoa wa Arusha.
Ili kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita.
Ilidaiwa siku ya tukio mwathirika akiwa njiani kuelekea nyumbani, mshtakiwa (mrufani) aliibuka kichakani akamtishia kwa panga, akamvuta kichakani akambaka na kumpora Sh18,000.
Mwathirika alidai kumtambua mshtakiwa kupitia vazi la asili la Kimasai. Baada ya tukio hilo alimjulisha shahidi wa tatu ambaye naye alimjulisha wa pili na kumkamata mshtakiwa aliyepelekwa ofisi ya mtendaji wa kijiji.
Ilidawa akiwa huko alisalimisha Sh18,000 na mwathirika wa tukio alimtambua katika ofisi hizo.
Mwathirika alipewa fomu ya polisi namba tatu (PF3). Shahidi wa nne aliyefanya uchunguzi wa kitabibu ulionyesha sehemu za siri za binti huyo zilikuwa na michubuko.
Licha ya mrufani kukana kutenda kosa hilo, alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Hakuridhika akakata rufaa Mahakama Kuu ambako alishindwa ndipo akakata nyingine Mahakama ya Rufaa akiwa na sababu saba ambazo majaji baada ya tathimini waliziunganisha katika hoja moja, kwamba kesi haikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Mrufani katika rufaa hiyo hakuwa na uwakilishi wa wakili, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule.
Upande wa Jamhuri uliunga mkono rufaa hiyo ukieleza kuhusu ukiukwaji wa taratibu kwamba, kwenye ukurasa wa nane wa rekodi ya rufaa iko kimya kuhusu jukumu alilokuwa nalo mkalimani katika kesi ya msingi.
Alidai jina la mkalimani halikutajwa lakini lilipelekwa na upande wa mashtaka na hakuapishwa. Haijulikani ni shahidi wa upande wa mashtaka wa nani alitafutwa mkalimani.
Wakili alieleza rekodi ilikuwa kimya iwapo mkalimani huyo alitelekeza jukumu lake kwa mujibu wa kifungu cha 227 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na kuamuru mahakama kutafuta mkalimani pia haikufuatwa, basi haiwezi kuhitimishwa kuwa kulikuwa na kesi ya haki.
Akitoa mfano wa shauri la Kigundu Francis na mwenzake dhidi ya Jamhuri (rufaa ya jinai namba 314/2010) aliomba mahakama kubatilisha hukumu hiyo.
Alieleza hata mkalimani angetekeleza jukumu la ukalimani kama inavyopaswa, bado ushahidi juu ya utambuzi wa macho kupitia vazi la kitamaduni la Kimasai ni utambuzi wa kimakosa, kwani hata mwathirika wa tukio hilo amesema naye alikuwa amevaa vazi la Kimasai.
Alidai rekodi haiko wazi iwapo mwathirika wa tukio hilo alimwelezea mrufani kwa shahidi wa pili na haijulikani nini kilisababisha kukamatwa kwa mrufani huyo.
Jaji Mdemu amesema kabla ya kupokewa ushahidi wa upande wa mashtaka katika mahakama ya chini, rekodi ya rufaa inaonyesha kulikuwa na dalili za kutumika kwa mkalimani katika kesi hiyo na kabla shahidi wa kwanza kuanza kutoa ushahidi wake ilielezwa mahakamani kuna mkalimani.
“Haijulikani tena ikiwa kizuizi cha lugha kilikuwa cha mshtakiwa au mashahidi wa upande wa mashtaka, vilevile haiko kwenye rekodi ikiwa mahakama iliamua kama mkalimani atatumiwa au la, kwa hivyo, wahusika walichagua kuendelea na kesi bila msaada wa mkalimani,” amesema.
Jaji Mdemu amesema kukosekana kwa uwazi huo katika rekodi ya rufaa ni maoni yao kuwa kesi iliendelea bila mkalimani wakati hilo ni kinyume cha kanuni za haki kwa hiyo imemuathiri mrufani.
Kuhusu utambuzi wa mrufani kupitia mavazi ya kitamaduni wamesema hayana msingi kwa sababu hata mwathirika wa tukio hilo alieleza alikuwa katika vazi hilohilo na mwathirika hakuwahi kumwelezea mrufani kwa mtu yoyote, hivyo haijulikani kwa nini mrufani alikamatwa.
Jaji Mdemu amesema ushahidi wa shahidi wa tatu ambaye anadaiwa kumtambua mrufani, unaacha maswali yasiyo na majibu kwani haijaelezwa iwapo siku hiyo, mrufani alikuwa amevaa mavazi yake ya kitamaduni ya Kimasai.
“Muhimu ni kwamba, mrufani alikuwa mgeni kwa mashahidi wote wa upande wa mashtaka, kama kwamba haitoshi, mashahidi wote wa upande wa mashtaka walidai kosa hilo lilifanyika katika Kijiji cha Ketumbaine,” amesema na kuongeza:
“Ushahidi ambao ulitofautiana kabisa na shtaka ambalo lilimkabili mrufani na kumbaka mwathiriwa ambayo inadaiwa ilitokea katika Kijiji cha Orkejuloongishu-Ketumbeine.”
Amesema baada ya kuzingatia dosari hizo wanakubaliana na wakili wa serikali kwamba, kwa masilahi ya haki, hii si kesi inayofaa kuamuru kusikilizwa tena.
Majaji wamehitimisha kwa kuruhusu rufaa, kufuta hatia, kuweka kando hukumu hiyo na kuamuru kuachiwa mrufani huyo isipokuwa kama atashikiliwa kwa sababu nyingine halali.