KAMATI ya Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa orodha ya mwisho ya majina ya wagombea 11 waliopenya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa shirikia hilo uliopangwa kufanyika Agosti 16, 2025, jijini Tanga.
Orodha hiyo ina majina ya wagombea 11 tu kati ya 25 waliojitokeza awali na kufyekwa kupitia hatua mbalimbali ikiwamo usaili uliofanyika mwezi uliopita uliokuwa na wagombea 19.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Uchaguzi, Wakili Kiomoni Kibamba zilionyesha majina ya wagombea katika nafasi mbalimbali ya urais ikiwa na jina moja la Wallace Karia anayetetea kiti chake.
Ukiachana na nafasi ya juu ya urais kwa wagombea wa ujumbe wa kamati ya utendaji wamegawanywa kuanzia Kanda ya Moja hadi Sita.
Nafasi ya Ujumbe Kanda namba moja waliopenya ni; Lameck Nyambaya na CPA Hosseah Hopaje Lugano, wakati Kanda namba mbili ina Khalid Abdahhal Mohamed pekee yake, ilihali Kanda namba tatu waliovuka salama ni James Patrick Mhagama, Evance Gerald Mgeusa na Cyrian Charles Kuyava.
Kanda ya namba nne ina mgombea mmoja tu, Mohamed Omar Aden, wakati kanda namba tano ina wagombea wawili, Vedastus Kalwira Lufano na Salum Alli Kulunge na kanda namba sita ina mgombea pia mmoja, Issa Mrisho Bukuku.
Awali kulikuwa na wasiwasi huenda uchaguzi huo ungeahirishwa kutokana na kuwepo kwa Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 inayoendelea nchini, Tanzania ikiwa wenyeji sambamba na Kenya na Uganda, lakini hadi sasa haijatangazwa mabadiliko yoyote ya tarehe kwa mujibu wa taaifa ya leo ya Kamati hiyo ya Uchaguzi.