Radi yaua watoto wawili, bibi ajeruhiwa

Mwanza. Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia na bibi yao kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi katika Mtaa wa Bulola ‘A’, Kata ya Buswelu, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea jana Agosti 7, 2025 saa 7:30 mchana wakati mvua iliyoambatana na upepo na ngurumo kubwa ilipoanza kunyesha.

Hali hiyo ikitokea, Grace Kateti (52), ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Bulola, alikuwa akipika chakula cha mchana chini ya mti jirani na nyumba yao akiwa na wajukuu zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha vifo vya watoto hao Mwasi Michael (11), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano na Charles Michael (6), mwanafunzi wa darasa la pili. Walikuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Bulola.

Kamanda Mutafungwa amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure.

Amesema Grace, ambaye ni bibi wa watoto hao alijeruhiwa na anaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Buzuruga.

Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kipindi cha mvua zinazoambatana na upepo na radi.

Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa Agosti 7, 2025 uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ilielezwa kuwa ni hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.