Samatta anatuheshimisha, ila sisi hatumheshimu

JUZI Jumatano ilikuwa siku ya furaha sana hapa kijiweni kwetu baada ya kusikia na kuona taarifa za nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kujiunga na Le Havre inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.

Sababu kubwa ya furaha yetu ni Samagol a.k.a Popat alishaonekana kama maji ya jioni na haikutegemewa kama angeweza kurudi katika ligi kubwa Ulaya kama ya Ufaransa akitokea Ugiriki alikokuwa akichezea PAOK.

Ilitarajiwa angebaki ama katika Ligi ya Ugiriki au angeenda ligi ambayo haina ushindani mkubwa, lakini mambo yameenda vizuri kwake kwani ametua katika moja ya ligi Tano Bora Ulaya.

Ni wiki kadhaa tu zilizopita tulishuhudia timu inayoshiriki Ligi ya Ufaransa ambayo ni PSG ikitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, mashindano ambayo yanaongoza kwa hadhi na thamani kwa ngazi ya klabu Ulaya.

Maana yake huko atakutana na mastaa wengi waliowahi kuvuma au wanaotamba katika mchezo huo hivi sasa kama Paul Pogba, Takumi Minamino, Bree Embolo, Andrew Ayew, Mohammed Salisu, Olivier Giroud, Ousmane Dembele, Marquinho, Vitinha na  Khvicha Kvaratskhelia.

Hili halitokei kwa bahati mbaya kwani linadhihirisha wazungu kuna kitu wanakiona katika miguu na kichwa cha Samatta, ndiyo maana leo hii licha ya umri alionao, timu inayocheza Ligi ya Ufaransa inaona haja na sababu za kumsajili na kuwaacha vijana wengi ambao baadhi wako kulekule Ufaransa.

Hata hivyo, wakati wenzetu wazungu wakiendelea kuamini katika ubora na daraja la Samatta kiuchezaji, mambo ni tofauti kwa hapa kwetu kwani mara kwa mara tumekuwa tukimchukulia poa nahodha wetu.

Zipo nyakati kadhaa tunamzomea na kumshambulia bila sababu Samatta na kuna wengine hadi hufikia hatua ya kumtukana jambo ambalo kuna baadhi ya nyakati humfanya mchezaji huyo kujiweka kando na timu ya taifa.

Lakini pamoja na sisi kutomheshimu, yeye amechagua kutuheshimisha sisi na nchi kijumla kwa kuzidi kupeperusha bendera yetu katika ligi mbalimbali.