Ahueni usafirishaji mizigo Zanzibar | Mwananchi

Unguja. Malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu mizigo yao kuchelewa kutokana na kukosa usafiri madhubuti, huenda yakapata jawabu baada ya ndege ya mizigo kuanza kuisafirisha kutoka Dubai kwenda moja kwa moja Zanzibar.

Ndege ya Solit Air aina ya Boeing 728 yenye uwezo wa kubeba tani 20 za mizigo, imewasilia kwa mara ya kwanza leo Agosti 9, 2025 kutoka nchi za Falme za Kiarabu.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Seif Abdalla Juma amesema hatua hiyo ni fursa siyo kwa Taifa kukuza uchumi, lakini kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha mizigo yao kuchelewa.

Amesema kuanza safari za ndege hiyo kunafanya kuwapo ndege tatu za mizigo zikiwamo za Shirika la Ndege Tanzania na Ethiopia.

Hata hivyo, ndege ya Solit Air ndiyo itakuwa inasafirisha mizigo moja kwa moja kutoka Dubai hadi Zanzibar.

“Kwa kweli hili ni jambo la kujivuani, jitihada hizi ni kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mizigo yao kwa wakati, wakiipata kwa wakati ndivyo itakavyochochea ukuaji wa uchumi, hata gharama za bidhaa zitapungua,” amesema.

Kwa mujibu wa Seif, Zanzibar imekua kwa kasi kubwa kupitia sekta ya ujenzi, biashara na utalii na mahitaji ya usafirishaji yameongezeka, hivyo Serikali inaendelea kufanya juhudi kwa upande wa bandari na viwanja vya ndege ambapo hivi sasa wafanyabiashara wana fursa ya kusafirisha mizigo yao ndani ya siku moja au mbili na kuendeleza biashara zao.

Amewataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo, kwani Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja ya Ndege inaendelea kuchukua juhudi na kuita mashirika mengi kupeleka ndege zake kwa ajili ya kusafirisha mizigo na abiria, hatua itakayoongeza ukuaji wa sekta za uchumi na utalii.

Lilian Erasmus, mkuu wa kitengo cha kukuza biashara na mawasiliano cha kampuni inayosimamia kuanza safari hizo ya Xerin Air Cargo, amesema ndege hiyo itakuja Zanzibar mara moja kwa wiki, ikitoa mizigo Dubai na kuleta Zanzibar na kutoa Zanzibar kupeleka Dubai.

Amesema lengo la kuleta ndege hiyo Zanzibar ni kuwasaidia wafanyabiashara wanaosafirisha mwani, samaki na bidhaa nyingine za mazao kutoka Zanzibar kwenda nchi za Falme za Kiarabu.

Vilevile kutoa fursa kwa wafanyabiashara na mawakala kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu nchini.

“Zanzibar kuna bidhaa nyingi ambazo zinakwenda nchi za Falme za Kiarabu hasa samaki, kaa, mwani na zinahitaji umakini wa hali ya juu wakati wa usafirishaji, lakini wengi wamekuwa wakikwama kwa hiyo baada ya kuona changamoto hiyo ikabidi kufanya utaratibu wa kuleta ndege itakayosaidia kutatua changamoto hiyo,” amesema.

Baadhi ya wafanyabaishara wanaosafirisha mizigo kwenda nje ya nchi wamepongeza hatua hiyo wakisema itawasaidia siyo tu kuwarahisishia usafirishaji, lakini itaongeza tija kwenye uchumi wa Taifa.

“Sisi tunapongeza ni hatua muhimu, ni ukweli usiopingika kulikuwa kuna changamoto za usafirishaji wa mizigo, mingi inatumia usafiri wa meli ambayo ni zaidi ya mwezi mmoja, lakini ukitumia ndege ndani ya wiki moja unakuwa umesafirisha na kuupata,” amesema Haji Ali Haji mmoja wa wafanyabaishara.