Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linafanya uchunguzi wa mauaji ya kijana ambaye hajafahamika jina, baada ya kukutwa ameuawa pembeni ya barabara katika Mtaa wa Malimbe, Kata ya Luchelele, Wilaya ya Nyamagana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea Agosti 9, 2025 ambapo mwili wa marehemu ulipatikana kando ya barabara ya Luchelele ukiwa na majeraha sehemu za mikononi na shingoni.
“Pembeni ya barabara alionekana mtu wa jinsia ya kiume ambaye anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30 akiwa amefariki huku mwili wake ukiwa utupu na majeraha mikononi, miguuni na shingoni.

Kamanda Mutafungwa amesema baada ya kupata taarifa hizo haraka walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi ili kubaini sababu ya kifo.
“Mwili wa marehemu ambaye hadi sasa umehifadhiwa katika Hospital ya Rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi zaidi, tukio hilo limekaguliwa na wataalamu wa matukio ya mauaji wa Jeshi la Polisi na uchunguzi unaendelea,” amesema Mutafungwa.
Mutafungwa amesema wakati wanafuatilia chanzo cha tukio hilo, ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na tukio hilo kuwasiliana na Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali au vyombo vingine vya usalama ili kusaidia kuwabaini wahusika.
Hofu kwa wakazi wa malimbe
Tukio hilo, liimeibua hofu kwa wakazi wa mtaa huo ambapo wameiomba Serikali iingilie kati ili kuleta usalama katika eneo hilo.
Mmoja wa mashuhuda, Anna Mwita ambaye ni mkazi wa eneo hilo, amesema alishtushwa na kundi la watu lililokusanyika kando ya barabara aliposogea akakuta ni mwanaume amefariki.
Aliiomba Serikali ifyeke msitu huo hatarishi ili kuondoa uhalifu unaojitokeza mara kwa mara.
Shuhuda mwingine, Janeth Andrea amesema eneo hilo limekuwa hatari kutokana na matukio yaliyowahi kujitokeza huku akiziomba taasisi zenye mamlaka ziliozopo karibu na eneo hilo kuimarisha usalama.
“Hichi kifo cha huyu kijana kimeniumiza sana na eneo hili limekuwa hatari sana,” amedai.
Mwanafunzi wa chuo kilichopo karibu na tukio lilipotokea, Hosea Raphael ameiomba Serikali kuongeza ulinzi shirikishi katika maeneo hayo ili kupunguza matukio yanayoendelea katika.
“Matukio kama haya yanatutia hofu kwa wakazi wa eneo hili, ukweli inatisha amani haipo, tunaomba Serikali iweke ulinzi shirikishi na askari waongeze ulinzi ili kupunguza matukio kama haya,” amesema.