:::::::::
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amepokea tiketi 10,000 za mashabiki watakaofika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, kushuhudia mechi ya Tanzania dhidi ya Madagascar inayotarajiwa kuchezwa leo, Agosti 9, 2025 majira ya saa 2 usiku.
Msigwa amepokea tiketi hizo Jijini Dar es Salaam, zikiwa zimebakia Saa chache kabla mechi hiyo kuanza, na kuwashukuru CRDB kwa kuwa miongoni mwa wadau wa mwanzo katika kuunga mkono juhudi za mwanamichezo namba moja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha uwanja unajaa kwa ajili ya Kuishangilia timu yetu ya Taifa Stars ambayo hadi sasa haijapoteza mchezo hata mmoja.
Pia Msingwa amewasihi wananchi na Mashabiki kutoka Maeneo mbalimbali nje na ndani ya Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi ili kuionesha Afrika kuwa hapa ni nyumbani kwa soka na huu ndio utayarisho wa Afcon hivyo ni vyema kuonesha picha nzuri ya ushirikiano na umoja wetu watanzania.
Naye Joseline Kamuhanda, Meneja wa Masoko wa benki hiyo amesema kuwa tiketi zitapatikana kwenye matawi ya benki hiyo, na kutaja matawi hayo ni Temeke, Mbagala, Buza, Tandika, Mbande, Ubungo, matawi ya Kariakoo na Posta, Kinyerezi pamoja na Mbande.