:::::::::::
Tanzania imeibuka mshindi wa pili katika maonesho ya kimataifa ya 97 ya kilimo na biashara yaliyofanyika Lusaka, Zambia kuanzia tarehe 29 Julai hadi 4 Agosti 2025.
Tanzania imetangazwa kuwa mshindi wa pili kati ya nchi 25 zilizoshiriki maonesho hayo ikitanguliwa na Zimbabwe iliyoshika nafasi ya kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Agosti 8, 2025 katika ukumbi wa MOI, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema ushindi wa Tanzania umetokana na maelezo ya kina na elimu iliyotolewa na wataalam kuhusu huduma za afya za kibingwa na kibobezi zinazopatikana Tanzania, pamoja na sekta ya usafirishaji.
“Taasisi tano zilishiriki katika maonesho hayo zikiwemo MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Rufaa ya kanda Mbeya (MZRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la ndege la ATCL, kwa ujumla wetu tumefanya vizuri na kushika nafasi ya pili” amesema Dkt. Mpoki
Amesema ushiriki wa Taasisi za afya kutoka Tanzania kwenye maonesho hayo umelenga kuhamasisha utalii tiba ili wagonjwa kutoka Zambia waje Tanzania kupata huduma badala ya kusafiri nje ya bara la Afrika kufuata huduma hizo kwa gharama kubwa.
“MOI na JKCI tunatoa matibabu ya zaidi ya asilimia 96 ya magonjwa yote ya moyo, mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu, hivyo ni kimbilio sahihi kwa bara la Afrika katika kupata matibabu bora na kwa gharama nafuu … tukiwa Zambia taasisi hizi tatu za afya tumeweza kuona watu 911 kati ya hao 105 wameahidi kuja Tanzania kwa matibabu zaidi” amesema Dkt. Mpoki
Ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo uliratibiwa na kusimamiwa na ubalozi wa Tanzania nchini Zambia chini ya Mhe. Balozi Lt. Gen Mathew Edward Mkingule ambapo pia banda hilo lilitembelewa na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichelema Agosti, 2, 2025.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba Tanzania Dkt. Peter Kisenge ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisis ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) amesema kamati hiyo imewekeza nguvu kubwa katika kujitangaza ili badala ya kupeleka wangojwa nje ya bara la Afrika kwa kufuata huduma bora na teknolojia ya hali ya juu, sasa wanapaswa kuwaleta wagonjwa wao Tanzania ambako huduma ni bora sawa na sehemu nyingine duniani.
“Awali tulienda visiwa vya Comoro na kutoa huduma kwa watu 2,292 na hadi leo tumepokea wagonjwa zaidi ya 150 katika hospitali zetu za MOI, MNH, JKCI na Ocean road, haya yote ni matunda ya ushiriki wetu kwenye maonesho kama haya” amesema Dkt. Kisenge na kuongeza kuwa
“Watu wanapoleta wagonjwa Tanzania wanasaidia kukuza uchumi wetu kwasababu watalala katika hoteli zetu, watanunua chakula na huduma zingine muhimu, hayo yote yatachagiza ukuaji wa uchumi na ndio maana tunaita tiba utalii kwa maana anatembea nchi yetu kwa ajili ya kupata matibabu”