BAADA kucheza mechi ya ndani na kombaini ya Arusha, kikosi cha Azam FC chini ya kocha Florent Ibenge kinaendelea na maanzalizi kikijifua kwa mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa Agosti 13 kabla ya kutimkia Rwanda.
Azam FC ipo Arusha ambako imeweka kambi kwa siku 14 na mipango yake ni baada ya siku hizo kwenda Rwanda kumalizia maandalizi ya msimu kabla ya kuvaana na Yanga, Septemba 11, 2025.
Inaelezwa kuwa kocha ameomba mechi mbili za ushindani kabla hawajaondoka Arusha na mpango tayari umefanyika kwa kuzungumza na JKT Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema kutakuwa na mchezo huo alioutaja kuwa sio sehemu ya mechi za ushindani, bali ni maandalizi ya kawaida.
“Ni kweli Agosti 13 tutakuwa na mchezo wa ndani wa kirafiki dhidi ya JKT Tanzania, lakini nakosa jina sahihi kuita mchezo wa kirafiki. Ni sehemu tu ya maandalizi, nafikiri mechi za kirafiki tutaenda kucheza Rwanda,” alisema Zakazi.
Kwa mujibu wa ratiba mchezo huo utapigwa Agosti 13 na siku moja ya kupumzika kabla ya kuanza safari kuondoka Arusha Agosti 15 kwenda Kigali, Rwanda, ambako watakaa hadi Agosti 30.