Joaquim Paciencia ndiye mkali wao

WAKATI zikiwa zimeshachezwa mechi 12 (kabla ya zile za jana) nyota wa Angola, Joaquim Paciencia ndiye mchezaji aliyefunga bao la mapema zaidi katika michuano ya CHAN 2024 inayoendelea katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zilizoandaa kwa pamoja.

Straika huyo anayeitumikia klabu ya Bravo do Maquis, alifunga bao dakika ya saba alipoitanguliza Angola mbele ya wenyeji Kenya na kumpiku Nasser Papus Ouattara wa Burkina Faso aliyekuwa akiongoza kwa bao la dakika ya 11 wakati nchi hiyo ikiizamisha Afrika ya Kati kwa mabao 4-2.

Hata hivyo, Kenya ilichomoa bao la Paciencia kupitia mkwaju wa penalti ya Austin Odhiambo na kufanya matokeo kuwa 1-1, lakini ikimfanya straika wa Kenya, kuwa kinara wa mabao kwa sasa akifikisha mawili, baada ya awali kufunga walipoizamisha DR Congo katika mechi ya ufunguzi.

Jumla ya mabao 23 hadi sasa yametinga wavuni (kabla ya mechi za jana) kupitia mechi 12, huku Wakati nyota wa Angola akiongoza kwa bao la mapema, Ange Zoumara wa Afrika ya Kati ndiye mchezaji aliyefunga bao la jioni zaidi akifunga dakika ya 90+5 wakati timu yake ikifa kwa mabao 4-2 mbele ya Burkina Faso akifuatiwa na beki wa Tanzania, Shomari Kapombe aliyefunga dakika ya 89.

Wakati Mkenya Austin Odhiambo akiongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao mawili, Quinito wa Angola ndiye mchezaji pekee aliyejifunga hadi sasa katika fainali hizo za CHAN 2024, pia kukiwa na mabao manne yaliyotokana na penalti, Burkina Faso ikiongoza kwa kufunga mikwaju miwili.

Abdoul Abass Guiro na  nahodha wa Burkina Faso, Patrick Malo ndio walioifanya nchi hiyo hadi sasa kuwa iliyofunga penalti nyingi, huku Abdul Suleiman ‘Sopu’ wa Tanzania akiwa mchezaji wa kwanza kufunga kwa penalti na wa kwanza kutupia katika fainali hizi za 8. Penalti ya nne ilifungwa juzi na Odhiambo, huku wachezaji wawili hadi sasa akiwamo nahodha wa Madagascar,Andriamirado Dax na Marvin Nabwire wa Kenya ndio walioonyeshwa kadi nyekundu hadi sasa.