ALIYEKUWA kiungo wa Simba, Sadio Kanoute anatarajia kuwasili nchini kesho alfajiri kwa ajili ya kujiunga na Azam FC.
Kanaute, raia wa Mali aliondoka nchini akiwa Simba baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu tangu msimu wa 2021-22 akitokea Al ahly Benghazi ya Libya ambapo punde tu baada ya kusajili alifanikiwa kupata namba kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Baada ya kutajwa sana kuwa atajiunga na Azam FC, Mkuu wa Idara ya Habari, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amethibitisha kuwa Kanoute anatarajiwa kuwasili saa tisa alfajiri.
“Kanoute anatarajia kutua nchini alfajiri ya kuamkia kesho saa 9:00 alfajiri,” ni sehemu ya maneno machache ya Zaka Zakazi.
Ujio wa Kanoute ndani ya Azam FC kwenye eneo la kiungo mkabaji kutamfanya mchezaji huyo aungane na mkongwe Himid Mao ambaye pia ametua katika dirisha hili la usajili.
Eneo hilo pia lina Sospeter Bajana, Adolph Mtasingwa, Yahya Zayd na Ever Meza.