Unguja. Baada ya kutoa malalamiko kuhusu fidia ndogo, wananchi wanaotakiwa kupisha mradi wa ujenzi wa barabara za mjini, likiwamo daraja la juu la Amani, Serikali imeagiza kufanyika mapitio ya tathmini iliyofanywa, ili kubaini uhalisia na kila mtu apate haki anayostahili.
Hatua hiyo imefikiwa leo Agosti 9, 2025 baada ya mawaziri watatu wanaohusika katika mchakato huo kukutana na wananchi kusikiliza changamoto zao na kutoa msimamo wa Serikali.
Baada ya mkutano huo, imebainika kuna hoja kwenye malalamiko yao, hivyo mawaziri wameagiza mthamini kupitia upya tathmini hiyo ndani ya wiki moja, ili Serikali ipate uhalisia wa jambo hilo.
Hivi karibuni wananchi hao wakizungumza na waandishi wa habari, walieleza kutoridhiswa na kiwango wanachotakiwa kulipwa, huku baadhi wakitakiwa kupewa kati ya Sh6 milioni na Sh15 milioni.
Mwa sasa mkandarasi wa Daraja la juu la Amani amesimama kuendelea na ujenzi kutokana na wananchi kutokubali viwango vya fidia na kukataa kusaini fedha hizo kupisha mradi.
Mawaziri waliokutana na wananchi ni Dk Khalid Mohamed wa Ujenzi, Mawasilino na Uchukuzi; Dk Saada Mkuya wa Fedha na Mipango na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Salha Mwinjuma.
Kilio kikubwa cha wananchi hao ni fidia ndogo wanayotakiwa kupewa baada ya kufanyiwa tathmini, wakidai viwango hivyo haviendani na uhalisia wa nyumba zao na hali halisi ya maisha kwa sasa.
Dk Mkuya amesema wakati tathmini hiyo inafanyika hakukuwa na mwongozo, ndiyo maana changamoto hizo zikaonekana, lakini sasa tayari umekwishatolewa.
“Kuna maeneo kweli kilichofanyiwa tathmini na kilichopo ni tofauti, kwa hiyo tumempa kazi mthamni apitie upya, ili kubaini mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi,” amesema.
Pia amesema wamebaini changamoto nyingine ya kutokuwapo uwazi wakati wa kufanya tathmini hiyo, kwamba wananchi husika hawakushirikishwa tangu hatua za awali.
Hata hivyo, amesema kuna watu walipewa hati za kujenga nyumba lakini wakajenga hadi maduka, kwa hiyo na wao wanataka kulipwa fedha, hivyo inaibua changamoto zingine.
Dk Khalid amesema wakati wanapitia upya tathmini hiyo, waendelee kujipanga kwa ajili ya kuhama, ili isije kufika hatua za mwisho ndipo wakaanza kutafuta utaratibu wa kuhama.
Amesem Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ana huruma na wananchi wake, ndiyo ameagiza wakutane nao, kisha kupitia malalamiko hayo ili kila mtu apate kinachostahiki.
Hata hivyo, Dk Khalid amesema si wananchi wote wanaweza kuridhika na fidia, lakini wanaamini hata kama mtu hajaridhika hapaswi kukataa, badala yake anatakiwa kuchukua fidia hiyo kisha aendelee na utaratibu wa kupeleka malalamiko kwenye kamati maalumu iliyoundwa na malalamiko yake yatafanyiwa kazi.
“Rais amekuwa akihimiza stahiki za wananchi ziwe sahihi, kwa hiyo niwaombe wananchi hakuna mtu atakayedhulumiwa, ndiyo maana tumekuja hapa, lakini tumeshaagiza mthamini arudie, ndani ya wiki moja na nusu ili tupate majibu sahihi,” amesema.
Hata hivyo, Dk Khalid amesema bado Serikali imetumia busara kuwalipa wananchi hao, kwani wengi wao wapo kwenye hifadhi ya barabara. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 2013, hifadhi ya barabara inatakiwa kuachwa mita 15 kutoka katikati ya barabara kila upande, lakini imekuwa tofauti wananchi wanajenga hadi kwenye hifadhi.
“Tujitayarishe kuondoka, tukimaliza kupitia mambo yakawa sawa isiwe tena nipewe miezi mitatu nijiandae kutoka, itafika mahali tunakwamisha mradi na mkandarasi, muda wake wa mkataba ukiisha atatushtaki na tunatakiwa kumlipa kwa sababu ya kuongeza muda,” amesema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilianza kujenga barabara za ndani zenye urefu wa kilomita 100.9 zikijumuisha madaraja mawili ya juu ya Mwanakwerekwe na Amani.
Ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya China CCECC ulianza Desemba mosi 2023 na ulitarajiwa kukamilika Machi 2025 kwa gharama ya Sh45 bilioni lakini ukaongezwa muda hadi Novemba 2026.
Awali, Abdalla Ali Salum, mmoja wa waliokumbwa na kadhia hiyo, amesema wao hawapingi maendeleo lakini wanataka kupewa kiwango cha fedha ambacho kinastahiki.
Mwananchi mwingine, Khadija Ali Salum, amesema nyumba yake ina vyumba vitatu na mlango mmoja wa duka, lakini baada ya tathmini anatakiwa kulipwa Sh6 milioni.
“Hizi fedha unaweza kuzifanyia nini, kwa kweli ni kilio kikubwa, lakini tunashukuru kwa kuwa Serikali imesema inakwenda kupitia upya kubaini tatizo, tunaamini itakuja na kinachostahiki tutalipwa na kupisha mradi,” amesema.
Maua Ali Salim amesema: “Kilio chetu tunaona kama kimesikika, hali ni mbaya, maana hapa unakuta wananchi wameshajijenga, kwa hiyo anapohama anakwenda kuanzisha maisha upya, sasa iwapo akipewa kiwango cha fedha ambacho hakifai inaumiza.”
Wananchi 128 wamefanyiwa tathmini katika eneo la daraja la juu la Amani ambapo Sh5.3 bilioni zimetengwa kuwalipa fidia kupisha mradi huo.