FURAHA na shangwe zilitawala kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Namboole, Kampala baada ya Uganda Cranes kupata ushindi wao wa kwanza kwenye michuano ya CHAN 2024, wakiiadhibu Guinea mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa Ijumaa usiku.
Bao la kwanza la Uganda lilifungwa dakika ya 31 na Regan Mpande, aliyetumia vyema krosi na kuupiga kichwa kilichomshinda kipa wa Guinea, Ousmane Camara.
Licha ya Guinea iliokuwa imeshinda bao 1-0 dhidi ya Niger kwenye mechi ya kwanza kujaribu kurudi mchezoni kwa pasi fupi na mashambulizi ya haraka, safu ya ulinzi ya Cranes ilibaki imara.
Fowadi wa Guinea, Yakhouba Barry, alipata nafasi nzuri muda mfupi baadaye lakini alishindwa kutumia nafasi hiyo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Guinea kushambulia kwa nguvu, lakini dakika ya 66 mambo yaliwaendea vibaya walipomwangusha Allan Okello kwenye eneo la hatari na mwamuzi aliamua ni penalti na Okello mwenyewe alifunga na kuipa Uganda bao la pili.
Guinea ilidhani imepata penalti dakika ya 74, lakini baada ya usaidizi wa VAR, uamuzi ukabatilishwa, kabla ya dakika ya 89, mchezaji aliyeingia kutokea benchi, Ivan Ahimbisibwe, kuihakikishia Uganda ushindi mnono kwa kufunga bao la tatu na kuzima matumaini ya wapinzani.
Kocha wa Uganda, Morley Byekwaso, hakuweza kuficha furaha yake baada ya mechi hiyo. “Nimefurahishwa na namna wachezaji walivyojibu mapigo. Kufunga mabao matatu na kushinda ni jambo la kujivunia. Tulirekebisha makosa ya mechi iliyopita, tukabadilisha baadhi ya wachezaji na matokeo yameonekana.”.
Byekwaso pia alishukuru mashabiki waliokuwa wakishangilia kwa nguvu muda wote: “Mashabiki walitupa presha kidogo, pia walitupa nguvu za kupambana hadi mwisho. Nawaomba waendelee kutuunga mkono.”
Katika mechi ya mapema kwenye kundi hilo C, Afrika Kusini ilipambana kutoka nyuma na kupata sare ya 1-1 dhidi ya Algeria, mabao yakifungwa na Abdennour Belhocini (Algeria, dakika ya 29) na Thabiso Kutumela (Afrika Kusini, dakika ya 45).
Baada ya matokeo haya, Algeria inaongoza Kundi C ikiwa na pointi 4, ikifuatiwa na Uganda yenye pointi 3 na tofauti nzuri ya mabao dhidi ya Guinea walio na pointi 3 pia. Afrika Kusini inashika nafasi ya nne na pointi moja huku Niger ikiwa mkiani bila pointi.