Kwa hizi mbinu za Folz, mjipange!

UNALIKUMBUKA balaa la Miguel Gamondi alipokuwa Yanga kwa aina ya soka lake lilivyotingisha kabla ya kuondoka? Jamaa alipotoka tu, akaingia Sead Ramovic akafanya balaa ndani ya muda mfupi na ile ‘gusa achia twende kwao’ kisha akasepa.

Mashabiki wa Yanga wakawa na presha baada ya kuondoka Ramovic, lakini akatua Miloud Hamdi na balaa la Gusa Achia Pro Max na kubeba makombe matatu kwa mpigo ndani ya muda mfupi na sasa buana, kuna huyu Romain Folz.

Kocha huyo Mfaransa kijana mwenye umri wa miaka 35, ndani ya wiki moja tu akiwa na kikosi hicho ameanza kufanya mambo kupitia mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kwa sasa jijini kuna vitu ameanza kuonyesha kutaka kuwashusha presha mabosi wa klabu hiyo.

Hii ni kwa falsafa alizoanza kuziingiza kwa mastaa wa timu hiyo inayoendelea kujifua kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam wakiwamo nyota wapya kama Andy Boyeli, Celestin Ecua, Balla Mousa Conte, Lassane Kouma, AbdulNasir Mohammed ‘Casemiro’, Abubakar Nizar ‘Ninju’ na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ sambamba na wale waliokuwa msimu uliopita.

Katika saa mbili tu ambazo Mwanaspoti limeyashuhudia, kocha huyo anataka wachezaji wake kugusa pasi moja ya fasta kisha kukimbia haraka kwenda kufunga. Ile staili yake ya ‘direct football’ inaonekana mapema. 

Yaani inapita mle mle walikopita kina Gamondi, Ramovic na Hamdi katika kuwakimbiza wapinzani na kama mastaa wa Yanga watashika vyema, ni wazi wapinzani wa timu hiyo wataendelea kupata tabu.

Linapofika jambo la mbinu hapo Folz anasimamia mwenyewe kazi hiyo, huku akiwatupa pembeni wasaidizi wake huku akikataa kabisa mambo ya mchezaji kukaa na mpira kwa muda mrefu, akitaka walisogelee lango la wapinzani haraka.

Huko mbele ya lango wachezaji wakifika kocha huyo hataki mambo mengi, yeye anataka kama unaweza kupiga, wewe piga shuti linalolenga lango na kama kufunga mtu afunge na sio kuleta madoido na kupoteza nafasi.

Katika mazoezi hayo washambuliaji Prince Dube na ingizo jipya Andy Boyeli wamekuwa wakifanya kweli kwa kufunga mabao mawili kila mmoja. Hata ukikosea Folz amekuwa kocha rafiki, kwani umuita mchezaji aliyekosea na kufanya mazungumzo mafupi naye palepale kwa utaratibu kisha kumpa nafasi ya kujirekebisha.

Kocha huyo alionekana kufanya hivyo kwa viungo Offen Chikola na Mohamed Doumbia katika mazoezi hayo akifanya nao mazungumzo mafupi, kisha akimaliza anapeana naye mkono na kazi inaendelea.

Aidha, kocha huyo anataka mara baada ya timu kupoteza mpira kazi ya haraka ni kutafuta kuurejesha katika himaya kwa kasi, jambo ambalo imewafanya wachezaji wengi kukimbia uwanjani muda wote. Kocha huyo amekuwa mkali kwa wachezaji wanaojaribu kutembea na alifanya hivyo akionyesha mkali kwa wachezaji wachache walioongezwa kutoka timu ya vijana ambao walionekana kujaribu kutembea.