TIMU ya taifa la Mauritania imeinyoosha Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa kundi B la mashindano ya CHAN 2024.
Bao hilo la mapema la dakika ya tisa kupitia kwa Ahmed lilitosha kuzima ndoto za Afrika ya Kati kutoboa katika kundi hilo.
Japokuwa Afrika ya Kati ilimiliki mpira zaidi kwa asilimia 57 dhidi ya asilimia 43 za Mauritania haikufua dafu mbele ya ngome imara ya Mauritania.
Afrika ya Kati ilipiga mashuti 16, lakini ni matatu ndiyo yaliyolenga lango. Ilikosa makali katika umaliziaji.
Mauritania haikupiga mashuti mengi – saba tu na la kwanza lililenga lango na ndilo lililozaa bao.
Ufanisi wa hali ya juu! Kocha wa Mauritania atakuwa na furaha jinsi vijana wake walivyotimiza majukumu yao.
Kwa matokeo hayo, Mauritania imefikisha pointi nne na kujikita nafasi ya pili kwenye kundi B, nyuma ya wenyeji Tanzania waliopo kileleni. Afrika ya Kati sasa wamenasa mkiani bila pointi, baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo.
Kwa mantiki hiyo, Afrika ya Kati inahitaji miujiza ili kufufua matumaini ya kusonga mbele.