Mtanzania aongeza uwekezaji katika saruji Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya mwekezaji kutoka Tanzania, Abdallah Munif kununua kampuni ya saruji ya Bamburi nchini Kenya, sasa ameongeza uwekezaji wake katika sekta ya saruji kwa kununua hisa kwenye kampuni nyingine ya East African Portland Cement (EAPC).

Munif kupitia kampuni yake ya Kalahari Cement iliyosajiliwa jijini Nairobi, amenunua asilimia 29.2 ya hisa za EAPC kutoka kwa Kampuni ya Uswisi, Holcim, kwa thamani ya KSh718.5 milioni (zaidi ya Sh12.54 bilioni).

Muamala huo unaosubiri idhini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Kenya (CMA), unamfanya Munif kuwa mmiliki mkubwa wa hisa za EAPC, akiwa na jumla ya asilimia 41.7.

Hisa hizo zinatokana na mashirika mawili yanayomilikiwa na Holcim Associated International Cement Ltd na Cementia Holding AG, kila moja kuuza asilimia 14.6.

Amenunua hisa hizo kwa bei ya KSh27.3 kila moja, ambayo ni punguzo la asilimia 42 ya bei ya soko la sasa KSh 47.5 (zaidi ya Sh914) katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE).

Hii ni hatua ya pili kubwa ya Munif ndani ya mwaka mmoja kwani mwaka jana, Amsons Group kampuni inayoongozwa na familia yake ilinunua asilimia 96.5 ya Bamburi Cement kutoka Holcim kwa gharama ya KSh23.5 bilioni (zaidi ya Sh452.54 bilioni).

Bamburi, tayari inamiliki asilimia 12.5 ya EAPC, jambo linalompa Munif ushawishi wa kipekee kwenye kampuni hizo mbili zinazoshikilia sehemu ya uzalishaji wa saruji nchini Kenya.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari inaeleza kuwa hatua hiyo inaifanya Amsons Group sasa kumiliki kampuni mbili zenye mitambo, ardhi ya ekari 909 za EAPC na mtandao wa masoko unaofika hadi Uganda.

Hili linafanyika wakati ambao EAPC imeshuhudia kuyumba kwa miaka mingi kutokana na changamoto za usimamizi na migogoro ya kiuongozi licha ya kuwa na historia ndefu.

Hali hiyo imeisababishia kuingia katika deni la KSh6 bilioni (zaidi ya Sh115.54 bilioni) pamoja na madeni kwa wafanyakazi na wasambazaji.

Holcim, Serikali ya Kenya inayomiliki asilimia 25.3 na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Kenya (NSSF) asilimia 27 zilishindwa kuirejesha kampuni hiyo kwenye faida.

Wachambuzi wanasema Munif ameona fursa ya kununua hisa hizo kwa punguzo, akiwa na mkakati wa kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama na kushindana na kampuni za Kichina zinazopanua shughuli zake katika kanda.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Edha Nahdi amesema mambo yako mezani kuhakikisha soko la Uganda linakamatwa.

“Uganda ni kama ndugu wa Kenya na Tanzania. Kila kitu kiko mezani,” amesema.

Kwa sasa, wadau wanasubiri kuona kama mikakati ya Amsons Group itaigeuza EAPC kuwa kampuni inayopata faida, jambo ambalo linaweza kuleta matokeo chanya katika bei ya saruji, ajira na ushindani katika kanda nzima.

Kwa mujibu wa African Cement Market Report 2024, mahitaji ya saruji Afrika Mashariki yanatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.3 kila mwaka hadi 2030, yakichochewa na miradi ya miundombinu, ujenzi wa makazi na ongezeko la miji.