Shinyanga. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Busalala, Kata ya Mwendakulima, Kahama mkoani Shinyanga Fatuma Khamis ameuawa kwa kuchomwa shingo na kitu cha ncha kali na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Agosti 9, 2025.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo.
Amesema watu hao ambao hawajafahamika wamemchoma mwalimu Fatuma na kitu chenye ncha kali upande wa kulia wa shingo yake.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Fatuma alikuwa na ugomvi wa kifamilia baina yake na mumewe na kwamba mpaka sasa wanamshikilia mume wa marehemu kwa uchunguzi zaidi.
Amesema, “aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali upande wa kulia wa shingo yake na watu wasiofahamika.
“Upelelezi wa awali palikuwa na ugomvi wa kifamilia, hivyo sasa hivi tunaendelea kupeleleza ili kuweza kujua nini kiini cha tukio hili, na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya manispaa ya Kahama.”
Amesema vitendo vya ukatili hususan wa kimwili, vimepungua mkoani humo na kwamba Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kutoa elimu kwa wanandoa kuepuka vitendo hivyo kwani ni kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa Nzengo ya Budushi Kata ya Mwendakulima, Richard Charles amesema alipata taarifa ya kifo hicho saa tisa usiku wa kuamkia leo kutoka kwa wananchi, ndipo alipofika eneo la tukio kutoa taarifa kwa viongozi wenzake.
Amesema hili ni tukio la tatu kutokea katika eneo lake ambapo tukio la kwanza mwanaume mmoja alishambuliwa kwa mapanga na kumsababishia kifo, la pili lilihusisha mwanamke mtu mzima kukatwa mapanga na watu wasiojulikana na hili la tatu kwenye Nzengo hiyo.
Ili kukabiliana nayo, amesema: “Sisi tumejipanga, kila jirani awe na namba ya mwenzie akisikia hata geti linaguswa ampigie simu.”
Naye Gervas Gabriel ambaye ni jirani wa marehemu, amesema tukio hilo limewahuzunisha kwani mwalimu huyo alikuwa ni mtu wa watu na ameiomba Serikali kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kufanya tukio hilo.
Mgambo wa Kata ya Mwendakulima, Philimon Nyanda amesema: “Kuna mtoto mdogo wa marehemu ambaye ana umri wa miaka minne aliamka akamkuta mama yake amelala chini na damu nyingi sana, akaenda kwa jirani na kuwaeleza kuwa ‘mama yangu amekufa nataka nilale kwenu silali tena kule’, ndipo majirani wakaamka na kufuatilia.”
Mwalimu mwenzake na marehemu, Rachel Isaac amesema, “sisi walimu tumesikitika kwa sababu mwalimu mwenzetu hakuwa na makuu na hiki kilichotokea Serikali iangalie maana tunaogopa yeyote linaweza kumkuta katika mazingira yetu ya kazi.”