Mwenge kukagua miradi 41 ya Sh25.9 bilioni Simiyu

Maswa. Mwenge wa uhuru wa mwaka 2025 utakagua, kuzindua, kutembelea na kufungua miradi 41 ya maendeleo yenye thamani ya Sh25.9 bilioni katika Mkoa wa Simiyu.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamring Macha amesema hayo leo jumamosi Agosti 9, 2025 katika kijiji cha Njiapanda wilaya ya Maswa mkoani humo wakati akikabidhiwa mwenge wa uhuru na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita.

Macha amesema ukiwa katika mkoa wa Simiyu, Mwenge wa uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 816.63 katika halmashauri sita za Maswa, Meatu, Itilima, Bariadi mji, Bariadi vijijini na Busega.

Amesema kuwa Mwenge wa uhuru unatarajia kuweka mawe ya msingi katika miradi12, kuzindua miradi11, kufungua miradi saba na kukagua na kuona miradi 11 yote yenye thamani ya Sh 25.9 bilioni.

“Nawashukuru sana na kuwapongeza wananchi wa mkoa wa Simiyu kwa kuibua kuanzish,kuchangia na kuitekeleza miadi hiyo ya maendeleo,”amesema

Pia, amesema kuwa mkoa huo umeshaanza maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025 kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwachagua viongozi ambao watawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Mkimbiza Mwenge kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura za mgombea urais,wabunge na madiwani ili maendeleo yaweze kupatikana.

Mkazi wa Kijiji cha Njiapanda Misonga Madauhu amesema wananchi wa eneo hilo wameupokea mwenge wa uhuru katika mbio zake za mwaka 2025.

“Kwa kuonyesha ya kuwa mwenge huu tumeupokea vizuri ni jinsi watu wengi walivyojitokeza kwa ajili ya kuushangilia pamoja na kuwepo kwa burudani mbalimbali za vikundi vya ngoma za asili pamoja na hamasa iliyofanywa na vijana wa skauti,” amesema.