Mzize alivyokaribia  rekodi hat-trick CHAN, akitupia mara mbili

STRAIKA wa Taifa Stars, Clement Mzize alikaribia kuweka  rekodi tamu kwa kuwa mchezaji wa nne kufunga mabao matatu yaani hat-trick  kwenye mechi moja ya mashindano ya CHAN.

Mzize mwenye miaka 21 amefunga mabao mawili  dhidi ya Madagascar kwenye mechi ya kundi B katika Uwanja wa Benjamini Mkapa  ambayo yameifanya Stars kuwa timu ya kwanza kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Stars imetinga robo fainali baada ya kufikisha pointi tisa kileleni huku ikiwa na mechi moja mkononi dhidi ya Afrika ya Kati ambayo inaburuza mkia kwa kuchapwa mechi mbili mfululizo.

Katika mechi dhidi ya Madagascar, Mzize alifungua akaunti ya mabao katika dakika ya 13 na 20 kabla ya Madagascar kuchomoja moja dakika ya 34 kupitia kwa Mika Razafimahatana.

Tangu kuanza kwa michuano hiyo miaka 15 iliyopita ni wachezaji watatu tu ambao wamewahi kupachika mabao matatu kwenye mechi moja.

Katika michuano ya kwanza ya CHAN 2009, mshambuliaji wa Zambia, Given Singuluma aliingia kwenye vitabu vya historia kwa kufunga hat-trick dhidi ya wenyeji Ivory Coast. 

Singuluma alimaliza kama mfungaji bora wa mashindano hayo kwa mabao matano.

Miaka saba baadaye,  2016 nchini Rwanda, Nigeria ilishuhudia nyota mpya akiwaka Chisom Chikatara, mshambuliaji wa Abia Warriors. 

Mshambuliaji huyo aliingia uwanjani kipindi cha pili na kufunga hat-trick  dhidi ya Niger  akiiongoza Nigeria kushinda 4-1.

Ingawa timu yao haikufika mbali, jina la Chikatara lilibaki midomoni mwa mashabiki.

Lakini mwaka 2018 aliibuka Ayoub El Kaabi wa Morocco. 

Katika kile kilichoitwa kampeni ya kihistoria, El Kaabi alifunga mabao manane katika mechi tano, ikiwa ni pamoja na hat-trick dhidi ya Guinea.