Sababu kipa Simba kutoenda kambini

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kwa mazoezi kambini jijini Ismailia, Misri kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano, lakini kuna kipa mmoja wa timu hiyo yupo Dar es Salaam na mwenyewe amefunguka sababu zilizomfanya asiwepo kambini na wenzake.

Kipa aliyekwama kuungana na wenzake kambini Misri ni Ally Salim ambaye amekuwa pia akiitumikia timu ya taifa, Taifa Stars na Mwanaspoti lilipozungumza naye jana amesema sababu kubwa ya kushindwa kuondoka ni ruksa aliyopewa ya kushugulikia matatizo ya kifamilia aliyonayo.

Hata hivyo, taarifa za awali ambazo gazeti hili lilizinasa ni kwamba kipa huyo alibakizwa kwa vile sio sehemu ya mipango ya kocha Fadlu Davids na kwamba yupo mbioni kutolewa kwa mkopo akihusishwa na klabu za Namungo na JKT Tanzania.

Lakini alipoulizwa juu ya tetesi hizo za kutolewa kwa mkopo kuwa sababu ya kumfanya asifuatane na wenzake Misri, Salim alisisitiza kwamba yeye bado ni mchezaji wa Simba na kama kuna lolote wenye mamlaka wa kulizungumzia ni waajiri wake.

“Kipindi cha usajili kina mambo mengi na lolote linaweza likatokea, lakini sababu niliyokupa kwa nini nipo Tanzania ni kushughulikia ishu ya familia, kila kitu kikikaa sawa nitaondoka kwenda kuungana na wenzangu Misri,” alisema Salim na kuongeza;

“Kikubwa ninachokiwaza katika kichwa changu ni namna ya kujiandaa na msimu ujao, ninaouona utakuwa mgumu, kutokana na timu zilivyosajili na zinavyofanya maandalizi yao.”

Mbali na hilo aliwazungumzia makipa wenzake Aishi Manula aliyejiunga na Azam FC, Beno Kakolanya anayehusishwa na Mbeya City pamoja na Moussa Camara kwamba yapo mambo aliyojifunza kwao.

“Ni makipa wazuri siwezi kutaja kila mmoja sifa zake, vipo vingi vilivyonijenga kutoka kwao, mfano kaka zangu Manula na Kakolanya walikuwa wananishauri kuendelea kupambana na kuniona nitafika mbali,” alisema.

Awali, zilikuwepo taarifa za ndani za Simba kutaka kumtoa kwa mkopo Salim aende Namungo, baadaye JKT Tanzania na endapo dili la Yakoub Suleiman likifanikiwa atakuwa mbadala wake.

Kulikuwa na mazungumzo baina ya uongozi wa Simba na JKT Tanzania ya kuhitaji huduma ya Yakoub mwenye mkataba wa miaka miwili, lakini bado mambo hayajakaa vizuri. Yakoub yuko na Taifa Stars sasa.