Sikia Diarra alichomfanyia Casemiro Yanga

PALE Yanga kuna mambo buana! Kuna maisha, lakini boli pia linatembea huku mastaa wageni wakinongesha chama hilo dhidi ya wenzao waliowakuta wakiendeleza vaibu kwa mashabiki wa chama hilo linalotarajia kuanza kutetea ubingwa wake mwezi ujao.

Tayari mastaa wa timu hiyo ambao hawapo katika mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), wameshaanza mazoezi chini ya benchi jipya la ufundi linaloongozwa na kocha mpya kijana Romain Folz aliyetua hivi karibuni kuwapa raha wana Jangwani.

Achana na hayo, kiungo mpya wa Yanga, Abdulnasser Mohamed ‘Casemiro’ amezungumzia mapokezi mazuri ndani ya uwanja kutoka kwa nyota wa kikosi hicho, huku akimtaja kipa Djigui Diarra kuwa amekuwa akimjenga na kuamini kwenye kipaji alichonacho.

Nyota huyo ambaye amekuwa akitajwa na mashabiki kuwa mchezaji bora, amejiunga na Yanga katika dirisha hili akitokea Mlandege ambayo imetwaa ubingwa wa Zanzibar alikotumika katika mechi zote 30 za msimu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Casemiro alisema amefurahia maisha ndani ya Yanga kwa siku chache alizopata nafasi ya kufanya mazoezi na timu huku akipokea ushauri mwingi na pongezi kutoka kwa watangulizi wake.

“Maisha ndani ya Yanga ni mazuri, nimepokewa vizuri. Ukiondoa kipaji changu ambacho kimewavutia wengi wamekuwa mstari wa mbele kunihusia ni namna gani natakiwa kujitunza. Nafurahi nimepata wachezaji viongozi,” alisema na kuongeza:

“Diarra ni kaka yangu na amekuwa rafiki. Tunazungumza mengi kuhusu soka na maisha nje ya mpira. Ananikubali sana sio yeye peke yake, lakini amekuwa karibu sana na mimi muda mwingi hasa wakati wa mazoezi.”

Mwanaspoti limeshuhudia kipande cha video cha kipa huyo namba moja wa Yanga akiwa na kiungo huyo na kumuuliza nini ambacho amekimwambia, na ndipo aliposema wamekuwa wakiongea mambo mengi.

“Ni mambo mengi nazungumza naye. Kubwa ameniambia kuwa nina kipaji kikubwa, natakiwa kujitunza na kutumia wakati huu wa maandalizi ya msimu kumuonyesha kocha mpya Romain Folz ambaye ndio kwanza anatengeneza timu yake ya ushindani,” alisema Casemiro.

“Kanisisitiza kuwa hata nikikosa nafasi ya kucheza sasa, natakiwa kuamini kuwa mimi ni mchezaji mkubwa na nina nafasi ya kufanya kitu kikubwa muda wowote nikipata nafasi. Amenijenga mambo mengi, nimemuahidi kuyafanyia kazi.”

Mchezaji huyo akizungumzia maandalizi kwa ujumla, alisema ni mazuri na yanatoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha kile alicho nacho na kilichobaki wanamuachia kocha ndiye atakayeamua.

“Nimeshuhudia ukubwa wa Yanga. Nimekutana na nyota wengi bora, licha ya mimi kutajwa kwa ubora kuna wachezaji wazuri na wananipa ushirikiano naiona timu hii ikiwa shindani msimu ujao.”