DROO ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu ujao tayari zimemalizika, ikishuhudiwa miamba ya soka nchini Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars zikipangwa kuanzia ugenini.
Mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na watani zao Simba iliyomaliza nafasi ya pili na kufuzu michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika, zitakutana na Wiliete Benguela ya Angola na Gaborone United ya Botswana mtawalia.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC iliyomaliza nafasi ya tatu, imepangwa kuanza dhidi ya EL Mereikh ya Sudan, huku Singida itakipiga na Rayon Sports ya Rwanda inayonolewa na Kocha Robertinho Oliviera aliyewahi kuinoa Simba.
Msimu uliopita Yanga iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wawakilishi wenzao kwenye michuano hiyo, Azam ikiishia hatua ya awali na sasa chini ya Kocha Florent Ibenge inasubiriwa kuona kama itaandika historia ya kufika hatua ya makundi iliyowahi kufikiwa na Namungo FC Kombe la Shirikisho.
Msimu uliopita pia ilishuhudiwa Simba ambayo imekuwa na rekodi nzuri katika michuano ya kimataifa, ikishiriki Kombe la Shirikisho, ilifika fainali na kuwa mshindi wa pili.
Hii ni mara ya kwanza kwa Singida kushiriki michuano ya kimataifa ikiipokea Coastal Union iliyoshiriki msimu uliopita, ikitabiriwa kufanya vyema kutokana na uwekezaji ilioufanya kwenye kikosi chini ya Kocha Miguel Gamondi aliyeifundisha Yanga na kufika nayo hatua ya makundi msimu uliopita.