BAADA ya droo ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika CAF kuchezeshwa hapa nchini, viongozi wa Simba na Yanga ambazo zinashiriki Ligi ya Mabingwa wamesema ziko tayari kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema maandalizi yanaendelea vizuri na kikosi hicho kipo tayari kupambana na kufanya vizuri.
“Tutajiandaa vizuri na tunaamini tutafanya vizuri Angola baada ya kurudi nyumbani pia, Mashindano yamekuja mapema zaidi na naamini tutafanya vizuri. Tuna malengo makubwa msimu huu ya Champions League,” amesema Hersi.
Kwa upande wake mjumbe wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesisitiza umuhimu wa kutodharau wapinzani, akitolea mfano mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy mwaka 2021
“Tumeshiriki kama wana fainali na hatuwezi kudharau timu yoyote. Kama utakumbuka vizuri, tulicheza na Galaxy ugenini tulishinda na tulipokuja hapa tukapoteza, mwaka uliopita tulicheza fainali na mwaka huu tumejiandaa vizuri,” alisema Try Again. Timu iko pre-season na tunaamini tutafanya vizuri,” amesema Try Again na kuongeza:
“Simba iko kwenye ubora wake na naamini hatutakuwa na kazi ngumu ya kuvuka hapa. Tumesajili wachezaji wazuri ambao tunaamini watatufikisha tunapopahitaji.”
Rais wa TFF, Wallace Karia amesema droo ya mashindano ya kimataifa kufanyika wakati wa michuano ya CHAN katika ukanda wa Afrika Mashariki ni heshima kubwa kwa taifa.
“Tumeweka historia nyingine kwa droo hii kufanyika wakati wa CHAN ambayo iko Afrika Mashariki. Hii siyo kwa upendeleo, ni kwa sababu tunastahili. Kwenye Champions League kuna timu mbili na hiyo pekee inatupa heshima kubwa,” amesema Karia.
“Vyote hivi vimetupa heshima Tanzania, na nikizungumzia droo iliyofanyika, inatupa picha ya jinsi tunavyoweza kuandika historia zaidi kwenye soka la Afrika Mashariki.”
Kocha wa timu ya taifa ya watu wenye ulemavu ‘Tembo Warriors’ Ivo Mapunda amesema kiufundi anaamini Simba na Yanga zinaweza kupenya hadi makundi ya Ligi ya Mabingwa.
“Mpira wa sasa umebadilika sina maana ya kuwa wapinzani wao ni wadogo mpira unaheshimiwa, lakini kwa viwnago vikubwa na ushindani unaoonyeshwa na Simba na Yanga wana nafasi kubwa ya kuvuka hapa na nawapa asilimia 70, 30 inabaki kwa wapinzani wao,” amesema Mpaunda na kuongeza:
“Ukiangalia Simba imekuwa na muendelezo kwenye mashindano haya, Yanga pia ilitolewa na Mamelodi kwa mikwaju ya penati unaona ni kiasi gani Tanzania ligi imekuwa.”