Sintofahamu kura ya maoni Bumbuli, uchunguzi unafanyika

Dar es Salaam. Wakati washindi wa kura ya maoni ya Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini wakisubiri hatima yao kutoka Kamati Kuu, mmoja wa watiania wa ubunge katika Jimbo la Bumbuli amelalamikia mwenendo usiofaa wa baadhi ya watiania wenzao walioshiriki kwenye kura ya maoni.

Wameeleza kwamba watiania hao walikiuka utaratibu uliowekwa na chama hicho, jambo linalohusishwa na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi huo, hivyo wanaziomba vyombo husika vichukue hatua kwa kufuatilia jambo hilo.

Agosti 4, 2025, watiania wa ubunge na udiwani nchi nzima walipigiwa kura na wajumbe ili kupata wagombea watakaokiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Katika Jimbo la Bumbuli, kinyang’anyiro cha kura ya maoni kilihusisha wagombea sita ambao ni Hidaya Kilima, Zahoro Hakuna, Ramadhani Singano, Rashid Kilua, Silas Shehemba pamoja na John Kilima.

Akizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wagombea kwenye kinyanganyiro hicho, amesema wakati wa wagombea kujitambulisha kwa wajumbe, chama kiliweka utaratibu kwamba wagombea wote watapanda gari moja kwenda kwenye kata.

Hata hivyo, amesema wagombea wawili waliokuwa wakishiriki uchaguzi huo, magari yao yalikuwa yakifuata nyuma msafara wa wagombea na wanapofika kwa wajumbe kujinadi, wakiondoka, magari hayo yanabaki na baada ya muda yanafuata tena eneo linguine walikoelekea wagombea.

“Sisi tunajiuliza haya magari ya wagombea wenzetu yalikuwa yanafuata nini wakati chama kimetuandalia gari la pamoja? Hizi zote ni rushwa, tunaomba vyombo vinavyohusika vichunguze hili na kuchukua hatua haraka,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya kwamba walikuwa pamoja na watiania hao kwenye gari la pamoja, lakini ndugu zao walikuwa kwenye magari yao na walipoulizwa walikiri kwamba kweli ni magari yao.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Lushoto, Nuru Mtoto amekiri kuwa na taarifa hizo, hata hivyo ametaka Mkuu wa Wilaya hiyo ndiyo atafutwe kwani ndiye mwenye vyombo vya ulinzi.

“Hili ni suala la Mkuu wa Wilaya kwa sababu ndiyo mwenye vyombo, mimi siwezi kuthibitisha. Hili suala niliambiwa lakini nimeliachia kwa sababu kuna vyombo. Wewe ukiongea na DC, yeye atakwambia kama kweli ilikuwa hivyo, yeye ndiyo anaweza kuthibitisha,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye amesisitiza kuwa CCM ni chama kinachozingatia kanuni na taratibu, na ndio maana wagombea wote walielekezwa kutumia usafiri wa pamoja ili kuondoa mazingira ya upendeleo au matumizi mabaya ya rasilimali.

Kuhusu madai ya rushwa, Sumaye amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa makini kuhakikisha hakuna mianya ya rushwa katika mchakato huo.

Amefafanua kuwa kesi chache zimeibuliwa dhidi ya watu wanaosadikiwa kutumwa na wagombea, ingawa bado uchunguzi unaendelea kubaini ukweli wa madai hayo.

“Wapo wanaodai wametumwa na wagombea lakini si kweli. Tukibaini ukweli kupitia uchunguzi, tutatoa taarifa rasmi,” ameongeza Sumaye.

Hata hivyo, jana Agosti 8, 2025, Katibu wa Itikati, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema hawajapokea malalamiko yoyote kuhusu mchakato wa uchaguzi uliofanyika