MSHAMBULIAJI nyota wa Algeria, Aimen Mahious, ameweka wazi dhamira yake ya kuiongoza timu yake kutwaa ubingwa wa CHAN 2024, akisisitiza kuwa huu ndio wakati wao wa kutimiza ndoto hiyo.
Katika mahojiano maalum na mtandao wa CAF, Mahious amefunguka kuhusu maumivu ya fainali ya mwaka 2022, matarajio yake binafsi, na shauku ya kurejesha heshima ya taifa hilo.
Mahious, ambaye ndiye mfungaji bora wa muda wote wa CHAN akiwa na mabao tisa, aling’ara kwenye michuano ya 2022, lakini akapata simanzi baada ya kukosa penalti ya kuamua ubingwa, hatua iliyowapa Senegal taji wakiwa wenyeji.
“Tulianza kwa nguvu na kupata alama tatu muhimu. Tunataka kuendeleza kiwango hiki au kukiboresha zaidi ili kuendelea kukusanya pointi,” alisema.
Kuhusu nafasi yake binafsi kama mfungaji, nyota huyo wa USM Alger alisisitiza kuwa malengo ya timu yana nafasi ya kwanza.
“Kipindi kilichopita nilipata tuzo ya mfungaji bora, lakini tulipoteza fainali. Safari hii nataka tuwe mabingwa,” aliongeza.
Mahious hakuepuka kugusia kumbukumbu mbaya ya penalti aliyoikosa mwaka 2022. Alikiri kwamba pengine alijiamini kupita kiasi, lakini sasa amejifunza.
“Soka ni maisha ya changamoto. Ukishindwa, unajipanga upya. Tuna nafasi mpya, na tutapambana hadi mwisho,” alisema.
Nchi tano tu zilizotwaa ubingwa wa michuano ya CHAN tangu ilipoasisiwa mwaka 2009, huku DR Congo na Morocco zikiwa pekee zilizotwaa mara mbili kila moja, wakati Libya, Senegal na Tunisia zikiwa zimebeba mara moja moja.
Algeria ambayo ni moja ya timu 19 zinazoshiriki fainali hizi zilizoandaliwa na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda imepangwa Kundi C ikiwa na Niger, Guinea na wenyeji Uganda iliyowanyoa 3-0 katika mechi ya ufunguzi na jana ilikuwa ikivaana na Afrika Kusini iliyokuwa ikicheza mechi ya kwanza.