Taifa Stars kanyaga twen’zetu robo

HAKUNA kitu kingine kinachosubiriwa na mashabiki wa soka nchini, ila kusikia na kuiona timu ya taifa, Taifa Stars ikivuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali ya michuano ya Ubingwa wa Nchi za Afrika (CHAN) 2024 kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.

Stars inayoongoza msimamo wa Kundi B ikiwa pia ndio wenyeji wa fainali hizo za nane ikiziandaa kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda, inashuka uwanjani leo Jumamosi kuanzia saa 2:00 usiku kukabiliana na Madagascar.

Mechi hiyo ya tatu kwa Stars na ya pili kwa Madagascar iliyoanza michuano hiyo kwa suluhu dhidi ya Mauritania utapigwe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ikitanguliwa na mechi ya mapema saa 11:00 jioni kati ya Afrika ya Kati na Mauritania.

Ushindi wa aina yoyote utaiweka timu hiyo katika nafsi nzuri ya kufuzu robo fainali na kuboresha zaidi rekodi ilizoweka hadi sasa katika michuano hiyo inayoshirikisha nchi 19 wakiwamo watetezi Senegal wanaotarajiwa kushuka uwanjani Jumanne ijayo visiwani Zanzibar kukabiliana na Congo Brazzaville.

Stars iliandika rekodi ya kwanza katika fainali hizo za CHAN 2024 kwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kuanza na ushindi katika michuano hiyo, kisha ikawasapraizi mashabiki kwa kushinda tena 1-0 mechi ya pili mfululizo dhidi ya Mauritania.

Matokeo hayo yakaifanya Stars kufikisha pointi sita na mabao matatu bila nyavu zao kuguswa ikiwa ni rekodi nyingine tamu ambayo haikuwahi kuandikwa kwa Tanzania kufikisha pointi sita katika mechi za makundi ya michuano yoyote ya Afrika hatua ya fainali kuanzia zile za AFCON hadi hizo za CHAN.

STR 01

Na leo sasa itakuwa na kazi mbele ya Madagascar ili kupata ushindi wa tatu mfululizo na kuboresha rekodi ya kuvuna pointi nyingi zaidi katika michuano ya CAF na kuvuka kwenda robo hatua ambayo haijawahi kufika katika historia ya nchi hii katika michuano yote ya Afrika tangu tupate Uhuru 1961.

Hata hivyo, Stars inapaswa kuwa makini mbele ya Madagascar wanaocheza kwa kujilinda na kushambulia kwa wakati mmoja na wenye rekodi ya kufanya vizuri mbele ya Tanzania katika mechi nne walizokutana tangu mwaka 2015, zikiwamo mbili za Cosafa na nyingine za kuwania Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar 2022.

Katika mechi zote mbili za Cosafa ikiwamo iliyopigwa hivi karibuni huko Afrika Kusini, Stars ilipoteza mbele ya Madagascar ikianza ile ya mwaka 2015 ilipolazwa mabao 2-0 na hiyo ya 2025 ilipolala 1-0.

Kwa mechi mbili za hatua ya makundi kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zilizopigwa mwaka 2021, Tanzania ilitakata kwa kushinda nyumbani mabao 3-2 kisha kwenda kulazimisha sare ya 1-1, japo haikuisaidia kusonga mbele kutoka Kundi J, lililoongozwa na DR Congo iliyomaliza na pointi 11.

Hivyo, leo itakuwa mechi ya kisasi baina ya timu zote, Madagascar ikisaka ushindi wa kwanza katika Kundi B, lakini Stars ikitaka kuendeleza dozi na kutanguliza mguu mmoja hatua ya robo fainali na kuandika historia katika michuano ya CAF.

STR 02

Stars inayonolewa na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ itakuwa na kazi ya kuibana Madagascar wanaocheza kwa mbinu, lakini ikijilinda vyema kama ilivyofanya mbele ya Mauritania licha ya ambapo licha ya kumpoteza nahodha wao Dax kwa kadi nyekundu, lakini ililazimisha suluhu mechi ya awali.

Lakini Stars imekuwa ikitengeneza nafasi lakini ikizipoteza, huku mabao mawili yakifungwa na mabeki ukiachilia penalti ya Abdul Suleiman ‘Sopu’, hivyo mechi ya leo ni wazi Kocha Morocco atakuwa ameshalifanyia kazi tatizo la safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ili kujitengeneza mazingira ya ushindi.

Hata hivyo usichokijua ni kwamba sehemu kubwa ya kikosi cha Stars wakiwamo mabeki wamefunga zaidi ya mabao 60 katika Ligi Kuu Bara iliyopita, akiwamo  Kapombe aliyemaliza na matatu kama Pascal Msindo, huku Ibrahim Bacca alifunga matano, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alifunga moja, Wilson Nangu (2) na Lusajo Mwaikenda alikuwa na sita akiwa ndiye kinara mwenye mabao mengi.

Katika eneo la mbele lina viungo na washambuliaji na waliokimbiza kwa mabao akiwamo Clement Mzize aliyefunga 14, Nassor Saadun (8), Idd Seleman ‘Nado’ (6), Mishamo David (5), Feisal Salum (4) huku Mudathir Yahya na Sopu kila mmoja akifunga matatu na kufanya safu ya mbele kumiliki mabao 43 dhidi ya 20 ya mabeki, ikiwa maana ukiondoka makipa wa timu hiyo, timu nzima inaweza kufunga.

STR 03

Katika pamoja jingine la kundi hilo itakayochezwa mapema, Afrika ya Kati itakuwa na kibarua ca kujiuuliza upya baada ya kuanza michuano kwa kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa Burkina Faso wakati itakapokabiliana na Mauritania kuanzia saa 11:00 jioni.

Ni mechi inayozikutanisha timu zilizotoka kupoteza mechi zao zilizopita kwani Mauritania ililala 1-0 kwa bao la Shomari Kapombe wa Tanzania dakika za lala salama, japo yenyewe inamiliki pointi moja iliyotokana na suluhu dhidi ya Madagascar. Nani atacheka au kulia mechi la leo? Ni suala la kusubiri.