Dar es Salaam. Katika hatua ya kudhibiti mapato, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuanza ukaguzi wa mita kubaini upotevu na wizi wa umeme unaofanywa na baadhi ya wateja.
Ukaguzi huo utakaofanyika nchi nzima utafanyika ikiwa ni siku chache tangu shirika hilo lije na mfumo wa kupokea taarifa za siri ili kuwabaini wahusika wa uhalifu ukiwamo wizi wa mali na uharibifu wa miundombinu.
Mfumo huo umeanzishwa ili kurahisisha upokeaji wa taarifa kutoka kwa wananchi, wafanyakazi wa Tanesco na wadau wengine kuhusu vitendo vya wizi wa mali za shirika, rushwa, hujuma za uharibifu wa miundombinu ya umeme na vitendo vya unyanyasaji visivyofaa katika mazingira ya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Agosti 9, 2025 iliyotolewa na Irene Gowelle, Kaimu Mkurugenzi wa mawasiliano na huduma kwa wateja, wapo baadhi ya wateja wasio waaminifu wanaochezea mita kuiba umeme ambao sasa mwisho wao umefika, kwani wakibainika wanaenda kukutana na mkono wa sheria.
Amesema hayo alipozindua ofisi ya huduma kwa wateja ya Kinondoni Kusini, iliyoko Kibamba ikiwa ni jitihada za kuendelea kuimarisha utoaji huduma na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi.
“Tumekuwa na changamoto ya upotevu wa mapato kutokana na mita zisizofanya kazi vizuri kutokana na umri lakini pia wako baadhi ya wateja ambao si waaminifu wamekuwa wakichezea mita kuiba umeme, sasa zoezi hili litahakikisha tunazikagua mita hizo na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watakaobainika ni wezi wa umeme,” amesema.
Pia ametoa rai kwa wananchi na wateja kutumia mfumo huo wa utoaji taarifa za siri kuwabaini na kuwafichua wanaolihujumu shirika hilo kwa kuiba umeme. Amesema shirika linahakikisha usalama na ulinzi kwa watoa taarifa.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Tanesco, mtaalamu wa biashara na uchumi, Dk Donath Olomi amesema mianya ikizibwa mapato ya shirika yataongezeka.
“Shirika kama hilo linapaswa kuwa na namna mbalimbali bunifu na njia za kubaini upotevu au wizi wa umeme na si kusubiri kitu cha kushtukiza inapaswa iwe endelevu,” amesema alipozungumza na Mwananchi kuhusu hatua hizo za Tanesco.
Amesema: “Hata maji pia yanapotea mashirika kama haya yanapaswa kuwa na vyanzo endelevu kwa kuwa siku hizi njia zipo nyingi, ikiwemo za kiteknolojia.”
Mkazi wa Dar es Salaam, Hassan Athumani amesema taarifa hiyo kwa wateja wasio waaminifu, wenye tabia ya wizi itawafanya waingiwe uoga hivyo wataiacha.
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano amesema upotevu husababisha shirika kutopata mapato halisi kulingana na kiasi cha umeme kinachozalishwa na gharama za kufikisha huduma hiyo kwa wateja.
“Ukaguzi vyema uwe sehemu ya kawaida ya majukumu hasa kwa kuanza na mita ambazo zinatiliwa shaka kimwenendo. Jambo hili vyema pia liambatane na mifumo ya kiuchunguzi maana wizi wa aina hii unaweza kuhusisha wadau wengi, wakiwemo vishoka na wenye upeo na uunganishaji umeme,” amesema.
Amesema ipo fursa ya kuboresha teknolojia pia ili kubaini upotevu katika mnyororo mzima wa umeme kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Gowelle, ameupongeza uongozi na wafanyakazi wa Mkoa wa Kinondoni Kusini kwa kuboresha mazingira ya ofisi hiyo.
“Uwepo wa ofisi hii mpya ni hatua muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Matatizo ya wateja sasa yatatatuliwa kwa haraka zaidi kwa kuwa tumesogeza huduma karibu nao,” amesema.
Gowelle amesisitiza matumizi sahihi ya umeme kama nishati salama na rafiki kwa mazingira katika shughuli za kupikia, akihamasisha wananchi kuunga mkono kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutumia nishati safi ya kupikia.
Ametoa rai kwa wafanyakazi wa ofisi hiyo kuipenda na kuitunza kwa uaminifu, sambamba na kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi.
Pia amesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya idara ya ufundi na ya huduma kwa wateja, pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu ili kuboresha zaidi huduma kwa wananchi.
Meneja wa Tanesco Kibamba, Salma Muharam, ametoa wito kwa wafanyakazi kuendelea kushirikiana ili kupunguza malalamiko ya wateja na kuhakikisha huduma bora zaidi zinatolewa.