::::::::
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limewataka wafanyabiashara waliopo ndani ya mkuza wa bomba la gesi asilia katika maeneo ya Kinyerezi Mwisho, hasa Mtaa wa Kanga na Kibaga, kuondoka katika eneo hilo kwa usalama wao na wa jamii kwa ujumla.
Katika kikao kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam, TPDC kupitia kwa Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi, Oscar Mwakasege, kililenga kuwaelimisha wafanyabiashara hao kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza endapo shughuli za kibinadamu, ikiwemo biashara, zitaendelea kufanyika ndani ya eneo hilo nyeti.
“Bomba la gesi linapita katika eneo hilo na kwa mujibu wa kanuni za usalama, hairuhusiwi kabisa kuwa na shughuli yoyote ya kibinadamu juu ya mkuza huo. Madhara ya ajali yanayoweza kutokea si tu kwa mtu binafsi, bali yanaweza kuathiri uchumi wa taifa kwa ujumla,” alifafanua Mwakasege.
Wafanyabiashara waliokutana na maafisa wa TPDC wameeleza kushukuru kwa kupata elimu hiyo kabla ya hatua za kuwaondoa rasmi kuanza. Wamesisitiza kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali lakini wakaiomba iharakishe uandaaji wa eneo mbadala la bwawa la Kanga, ambalo limetengwa kwa ajili ya shughuli zao za kibiashara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kanga, Shamte Mkali, alisema kuwa tayari hatua za awali za maandalizi katika eneo hilo jipya zimeanza, zikiwemo kazi za ujazaji wa kifusi ili kuandaa mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
“Kutokana na maombi yao, serikali ilikubali kulitenga eneo la bwawa la Kanga kwa ajili ya biashara. Tayari tumeanza kulifanyia kazi ili kuhakikisha wanaondoka salama na wanaendelea na shughuli zao kwa utulivu,” alisema Mkali.
Hatua hii ya TPDC ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama wa wananchi na miundombinu muhimu ya kitaifa, sambamba na kutoa suluhisho endelevu kwa shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo hatarishi.
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY