Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Kampeni ya Elimu ya Kodi kwa Biashara za Mtandaoni kwa lengo la kuhakikisha kila anayehusika na biashara hizo anajisajili ili aanze kulipa Kodi.
Akizindua kampeni hiyo leo tarehe 09.08.2025 Jijini Dar es Salaam Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema wanaolengwa katika usajili huo ni Wafanyabiashara wenye kipato cha zaidi ya Sh. Milioni 4 kwa mwaka ambao Kodi yao itakuwa Sh. 100,000 kwa mwaka na kila mmoja atalipa kulingana na kipato chake.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema wakati wakiendelea kutoa Elimu kwa Wafanyabiashara wote wanaofanya biashara za mtandaoni kujisajili, wataanza na wanaofanya biashara ya kukodisha nyumba mtandaoni pamoja na wale wanaoendesha biashara mtao ambao wamekuwa wakipata fedha nyingi na hawalipi Kodi.
Amesema TRA itatoa asilimia 3 ya Kodi itakayookolewa kwa watu watakaotoa taarifa za ukwepaji wa Kodi kwa Wafanyabiashara watakaoshindwa kujisajili ndani ya muda uliowekwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wanaokwepa Kodi na watawatambua kwa kutokutoa risiti.
“Kila anayestahili kulipa Kodi atalipa kulingana na uwezo wake na mtaji wake na tupo kwaajili ya kuwezesha biashara hivyo hakuna mtu atakayeonewa katika utozaji wa Kodi” amesema Mwenda.
Amesema ili kuwezesha biashara wanaanzisha kitengo cha kuwezesha biashara katika kila mkoa wa Kodi kitakachosaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara na kutatua changamoto za Walipakodi ili kuwawezesha kulipa Kodi kwa hiari.
I