Tshabalala amliza Mtunisia | Mwanaspoti

YANGA imemsajili na kumtambulisha beki wa kushoto wa zamani wa Kagera Sugar na Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, anayeendelea na majukumu ya kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars inayoshiriki michuano ya CHAN 2024, lakini kuna kocha mmoja ameshtushwa na usajili huo.

Tshabalala aliyeitumikia Simba kwa misimu 11 tangu 2014 alipotua akitokea Kagera Sugar amepewa mkataba wa miaka miwili kwa dau la maana, lakini kabla ya dili hilo kutiki Yanga, kuna kocha alikuwa akimvizia ambebe na baada ya kumkosa amekiri ameumia, japo amewafagilia Wananchi kwa kumnasa.

Kocha Nasreddine Nabi aliyewahi kuinoa Yanga, amewapongeza mabosi wake wa zamani kwa kuipata saini ya Tshabalala, huku akifichua siri kwamba klabu hiyo ilikuwa ikimpigia hesabu kitambo ila ugumu ulikuwa kwa Simba.

Nabi aliyepo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu alisema, moja kati ya wachezaji wazuri na wenye uzoefu ambao Yanga imewasajili msimu huu ni wa Tshabalala.

Alisema kuwa, timu hiyo imepata beki mzuri ambaye yupo katika daraja la ukomavu mkubwa na anaamini anakwenda kuimarisha upande wa kushoto wa kikosi hicho.

“Tangu alipokuja Joyce Lomalisa, Yanga ilikuwa na mipango ya kumsajili Tshabalala kwa lengo la kuimarisha zaidi eneo la kushoto, mpango ambao haukufanikiwa,” alisema Nabi na kuongeza; 

“Yanga ilikuwa inampigia hesabu ya kumpata Tshabalala kwa muda mrefu, lakini ilikuwa ngumu kumchukua kutoka Simba ila hata mimi nilitamani kuwa na beki kama huyo,” alisema Nabi. 

Mwanaspoti iliwahi kuripoti kuwa kati ya timu ambazo zilikuwa zikiwania saini ya mchezaji huyo ni Kaizer Chiefs, lakini Simba iliwakazia kumpata.

“Simba iligoma wakati Kaizer inamtaka, baadaye tukakutana na ugumu wa kufikisha idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, ila ni mchezaji ambaye ataongeza kitu kikubwa ndani ya Yanga, hasa kwenye uimara wa kuzuia na hata kushambulia,” alisema Nabi aliyeinoa Yanga kwa miaka miwili na nusu na kuipa mafanikio makubwa ikiwamo kuweka rekodi ya kubeba ubingwa bila kupoteza mchezo wowote.

Tshablala anakwenda kucheza nafasi moja na Chadrack Boka ambaye alianza kuitumikia Yanga msimu uliopita akitokea Lupopo, huko ujio wake ukimweka benchi Nickson Kibabage.