Unguja. Mtiania wa urais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina amesema wanakweda kuandika historia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiahidi Watanzania kunufaika na rasilimali za nchi.
Kwa upande wake, mtiania wa urais wa Zanzibar, Othman Masoud amesema uchaguzi wa Oktoba ndiyo wakati sahihi wa kuiondoa CCM ili kurejesha heshima ya kisiwa hicho, akiwataka wananchi kuiunga mkono ACT-Wazalendo.
Mpina aliyejiunga na ACT-Wazalendo akitokea CCM hivi karibuni, amesema Serikali chini yake na Othman, mambo yote yaliyokwama yatakwenda kukwamuliwa ili rasilimali za Taifa zinawanufaishe Watanzania.

Wameeleza hayo leo Jumamosi Agosti 9, 2025 katika uwanja wa Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Michenzani mjini Unguja, baada ya kupokewa ikiwa ni ishara ya kujitambulisha baada ya kupitishwa na chama hicho kuwania nafasi hizo Agosti 6, 2025 kwenye mkutano mkuu.
“Tunagombea nafasi hizi si kwa kutaka vyeo bali kwenda kutatua changamoto za Watanzania ambazo suluhisho pekee ni ACT-Wazalendo kilichowaletea wagombea bora watakaotatua kero zote zilizoshindikana,” amesema Mpina.
Amesema kitendo cha chama hicho kumpa nafasi ya kupeperusha bendera ya urais, hawajakosea kwa sababu chama hicho kimejikita katika masilahi ya watu.
“Wanajua kabisa Mpina, muda na saa zote masilahi yake ni kupigania Taifa letu hadi kuhakikisha linafikia maendeleo yanayotamaniwa na Watanzania wote,” amesema na kuongeza:
“Niwahakikishie viongozi na wanachama wa ACT-Wazalendo kuwa hapa mmepata mwanachama (Mpina). Mkinichagua kuwa Rais basi, kiongozi mmepata,” amesema huku akishangiliwa.
Kuhusu Fatma Albdulhabib Ferej ambaye ni mgombea mwenza wa urais, Mpina amesema: “Namwamini sana Ferej ni jembe na Watanzania watapata kiongozi bora endapo watafanikisha kuingia Ikulu, Oktoba.”
Mpina amesema kwa ngazi aliyoifikia Othman hadhi yake ni kuwa Rais wa Zanzibar siyo Makamu wa Rais kutokana na uzalendo na uchapakazi wake, akiwaomba wananchi kumuunga mkono.
“Mapokezi mliotupa yametupa heshima kubwa, sikujua kama itakuwa hivi, kila nikiangalia pande zote watu wamefurika. Heshima hii tafsri yake watu wa Zanzibar mnakipenda na kukithamini chama cha ACT- Wazalendo,” amesema Mpina na kuongeza:

Umati wa wananchi na wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, mjini Unguja wamefurika kuwapokea watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Luhaga Mpina na Othman Masoud (Zanzibar) waliokwenda kujitambulisha.
“Tasfiri ya pili mmedhihirisha kwamba, chama hiki kimewaletea watiania wazuri na mwisho mapokezi haya yanamaanisha Othman anakubalika.”
Katika mkutano huo, Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi kujiandaa na uchaguzi utakaofanyika Oktoba kuindoa CCM madarakani ili kurejesha haki na heshima ya Zanzibar.
“Tunakokwenda, hatuendi kwenye uchaguzi kwa sababu ya kuitafutia ACT-Wazalendo Serikali au kumpa Othman Masoud urais, bali kutafuta heshima ya Wazanzibari,” amesema na kuongeza:
“Tunakwenda kutafuta haki na heshima ya Wazanzibari iliyopotea ili kuirejesha, lazima tuwarejeshee wananchi ufalme wao, kwa hili… Tunakokwenda ni kukugumu lakini ndiyo vizuri ili tufanikiwe,” amesema Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema mapokezi hayo yanaashiria chama hicho kitaibuka kidedea katika uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Amesema watiania waliopendekezwa kuwania nafasi hizo wamepatikana baada ya wajumbe wa mkutano mkuu maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 6, 2025 kuwathibitisha na kuwapitisha kupeperusha bendera ya chama hicho.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo walimpitisha Mpina kwa kura 559 sawa na asilimia 92.3 dhidi ya mshindani wake Aaron Kalikawe aliyepata kura 46 sawa na asilimia 7.7
Wakati Othman aliyekuwa mtiania pekee alipigiwa kura za ‘Ndiyo’ 606 sawa asilimia 99.5 ya kura zote zilizopigwa.
“Haya ndiyo majembe yatakayoitoa CCM kuanzia hapa Zanzibar hadi Tanzania Bara,” amesema Ado huku akishangiliwa.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amewashukuru Wazanzibari kwa kujitokeza katika mapokezi hayo, akisema hizo ni salama kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa chama hicho kipo tayari.
“ACT-Wazalendo kipo na umma kwa bega kwa bega, tunaitaka ZEC (Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar) kutenda haki katika uchaguzi Oktoba. Umma huu uliojitokeza upoa tayari kwa uchaguzi,” amesema.
Kwa upande wake, Ferej amesema 2025 ni mwaka wa mabadiliko, akisema umma huo uliojitokeza kuwalaki unaonyesha upendo mkubwa kwa watiania waliokwenda kujitambulisha.
“Niwahakikishe Mpina ni kiongozi, niliwahi kufanya naye kazi tukiwa bungeni ni sauti ya wanyonge inayopinga ufisadi nchini. Mpina ndiye atakayekuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili Watanzania,” amesema na kuongeza:
“Naomba muiamini timu hii haitawaangusha, nitatumia uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 20 kusaka kura jimbo kwa jimbo.”
Ferej ametuma salamu kwa INEC na ZEC akizitaka taasisi hizo kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki kwa vyama vyote vitakavyoshiriki uchaguzi Oktoba mwaka huu.
Awali, saa 4:10 asubuhi safari ya matembezi ya kuwatambulisha watiania hao ilianza eneo la bandarini ambako Othman, Mpina na Ferej walipanda gari moja la wazi na mbele yao walisindikizwa na viongozi waandamizi wa chama hicho.
Njiani walipungia mikono wananchi na wachama wa ACT-Wazalendo waliojitokeza kuwalaki wakati msafara wao ukipita.
Msafara huo uliosindikizwa na matarumbeta na muziki uliopigwa kutokea gari la matangazo ulilazimika kusima katika baadhi ya maeneo kusalimia wananchi.
Maeneo ambayo msafara huo umesimama ni Malindi, Soko la Darajani, makutano ya mataa ya Mkunazini, Kisiwandui hadi Kisonge, ambako walishuka na kutembea kwa miguu hadi ‘Mnarani square’ ambako matembezi yalihitimishwa yakichukua takribani dakika 50.
Kutokana na umati uliokuwapo uliofuatana na msafara huo, barabara za kuelekea bandarini, Darajani hadi viwanja vya Mnazi Mmoja na Maisara zimefungwa kwa muda.