Waombolezaji 25 wafariki dunia ajalini

Dar es Salaam. Watu 25 wamefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi la shule lililowabeba waombolezaji katika eneo la Mamboleo Coptic, Kaunti ya Kisumu, nchini Kenya.

Kwa mujibu wa mitandao ya kijamii nchini Kenya, ajali hiyo imetokea Agosti 8, 2025 ikielezwa uchunguzi wa awali umebaini dereva alipoteza udhibiti wa basi hilo kwenye sehemu ya barabara ambayo ajali hutokea mara kwa mara.

Imeelezwa basi hilo lililokuwa limebeba waombolezaji wakirejea nyumbani kutoka kwenye mazishi Kusini-Magharibi mwa Kenya lilipinduka hadi kwenye mtaro na kusababisha vifo vya watu 25.

Dereva alishindwa kulidhibiti basi hilo lilipokaribia mzunguko wa barabara likiwa katika mwendo kasi, hivyo likatumbukia kwenye mtaro.

Kwa mujibu wa Peter Maina, ofisa wa usalama wa barabarani katika Mkoa wa Nyanza: “Gari lilipoteza udhibiti, likapinduka na kubiringita upande wa pili wa barabara.”

Fredrick Olunga, katibu mkuu anayesimamia huduma za matibabu nchini Kenya amesema watu 21 walifariki dunia eneo la tukio, huku wanne walikufa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) Ijumaa usiku Agosti 8, Olunga amesema majeruhi 28, akiwamo mtoto wamelazwa kwa ajili ya matibabu.

“Tumewakusanya wahudumu wote wa afya walio zamu na kuwatahadharisha wafanyakazi wa ziada ili kuhakikisha waliojeruhiwa wanapata huduma bora zaidi,” amesema.

Ili kuokoa maisha ya majeruhi kumeandaliwa utaratibu wa watu kutoa damu kuanzia leo Agosti 9 katika Hospitali ya JOOTRH.

“Pia tunafanya kazi kwa karibu na serikali ya kaunti na hospitali zinazozunguka ili kukabiliana na ajali hii. Shughuli za uchangiaji damu tayari zinaendelea,” amesema na kuongeza:

“Hii ni mbaya kwa taifa zima. Tunasimama pamoja na familia zilizofiwa na tunawatakia majeruhi ahueni ya haraka.”

Hii si ajali ya kwanza katika eneo hilo, Julai 31, 2024 lori lililojaa mbao lilipinduka eneo la Mamboleo (Coptic area), watu wawili walikufa papo hapo.

Julai 15, 2024 basi la chuo lilipinduka likikaribia eneo hilo na kusababisha kifo cha mwalimu mmoja, huku wanafunzi kadhaa wakijeruhiwa.

Aprili mosi, 2024 ajali ya basi ilitokea eneo hilo likiwa linasafirisha wanafunzi, mmoja alifariki dunia na wengine walijeruhiwa.