ZEC kutangaza ratiba ya uchaguzi Agosti 18, kusaini maadili Agosti 24

Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), wakati ikiendelea na matayarisho ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, imesema itatangaza ratiba ya uchaguzi huo Agosti 18, 2025.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 2018 inawataka watangaze ratiba ya uchaguzi siku tano baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi ambapo baraza linatarajiwa kuvunjwa Agosti 13, 2025 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 9, 2025 na  Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya wilaya kuwajengea uwezo.

“Inatakiwa tutangaze ratiba ndani ya siku tano na sio zaidi ya siku 21 baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo tunatarajia kutangaza siku tano baada ya baraza kuvunjwa, hivyo Agosti 18 tutatoa kalenda nzima ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” amesema Faina.

Ratiba hiyo itakuwa ni pamoja na uchukuaji wa fomu, urejeshaji wa fomu na tarehe ya uteuzi wa wagombea.

Faina amesema baada ya kutangazwa ratiba hiyo, hatua itakayofuata ni kusaini maadili ya kampeni ambayo yanatarajiwa kusainiwa Agosti 24 mwaka huu.

Amesema safari hii watasaini kwa aina yake kwa kuanda matembezi maalumu ya kuhamasisha amani kutoka Ukumbi wa Idrissa Abduwakil Kikwajuni hadi Maisara zilzipo ofisi za Tume hiyo, lengo ni kuhamasisha amani katika uchaguzi huo.

Amesema baada ya kufika katika ofisi za Tume, kazi hiyo itafanywa kwa kusaini maadili ya kampeni ya uchaguzi.

Awali, wakati akifungua mafunzo hayo, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji George Joseph Kazi, amesema mafanikio ya tume hiyo kutekeleza takwa la kisheria kifungu cha 34 cha sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 la kuwajibika kuendesha uchaguzi mkuu wanalo wasimamizi hao kwani ndio kiungo muhimu kati ya ZEC na jamii.

Amesema wao wanafanya kazi kwa niaba ya tume hivyo katika mazingira ya kisasa na kijamii, uchaguzi si tu tukio la kisiasa bali linaweza kuathiri amani, maendeleo na mshikamano wa taifa.

“Kukosekana kwa maandalizi madhubuti au uzembe katika usimamizi wa uchaguzi kunaweza kusababisha migogoro, kupotea kwa imani ya wananchi juu ya taasisi yao hiyo muhimu,” amesema.

Amebainisha kuwa katika maeneo yao huko ndipo kura zitakapopigwa na kuhesabiwa na kufanyika majumuisho hivyo wao wanawajibika kuwa na uwezo wa kutosha unaoendana na uwelewa wa masuala yote muhimu ya uchaguzi katika kipindi hiki.

“Uwezo na uwelewa wenu naamini ndio itakuwa njia sahihi ya kuelekea katika mafanikio ya kutekeleza majukumu yenu,tunawategemea kuwa mfano wa kuigwa kwa maadili ya kazi, nidhamu, na uwajibikaji na lazima mtuthibitishie kuwa ZEC ni taasisi inayoweka mbele maslahi ya umma na inayosimamia uchaguzi kwa haki bila upendeleo,” alisema.
Hata hivyo, aliwasisitiza kutumia muda wao kusoma sheria, kanuni na miongozo waweze kufanya kazi zao kwa mafanikio.
Amesema kwamba baada ya kupatiwa mafunzo hayo wana wajibu wa kuyashusha kwa wasaidizi wao watakaosimamia uchaguzi katika ngazi za majimbo na vituo vya uchaguzi.