Angola yapindua meza kibabe, ikiizima Zambia

Angola imetoka nyuma na kutengeneza ushindi muhimu mbele ya Zambia, ikishinda kwa mabao 2-1 katika mchezo wa tatu hatua ya makundi ya Fainali za Ubingwa kwa Mataifa Afrika (CHAN) 2024.

Zambia iliyokuwa ikicheza mechi ya pili, iliyokuwa ya kwanza kupata bao baada ya timu hizo kumaliza dakika 45 za kwanza zikiwa hazijafungana, mfungaji akiwa Dominic Chanda dakika ya 73.

Bao hilo lilitokana na  shambulizi lililozalishwa na mpira wa friikiki ukipigwa na nahodha wa timu hiyo, Kelvin Kampamba.

Dakika sita baadaye Angola ilisawazisha bao hilo kupitia Joao Manha akimalizia kazi nzuri ya winga wa kulia, Joao Maunha.

Ni kama vile mabaonya Angola yalikuwa benchi baada ya Manha na Maunha kuingia kipindi cha pili dakika ya 61 kisha kuja kuipa ushindi timu hiyo.

Alikuwa ni Manha tena aliyefunga bao la pili akimalizia kazi ya Maunha na kujihakikishia ushindi nchi hiyo, ukiwa ni wa kwanza katika fainali hizo za nane tangu 2009.

Ushindi huo ulipatikana kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi unaifanya Angola kufikisha pointi nne katika kundi A, nyuma ya wenyeji Kenya inayoongoza kwa  pointi saba kila moja ikicheza mechi tatu.

Morocco ambao ilishtuliwa mapema leo jioni kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kenya, ipo nafasi ya tatu na pointi  tatu sawa na DR Congo, huku Zambia ikiburuza mkiani bila pointi yoyote kutokana na kupoteza mechi mbili za kwanza.