AZAM FC imeendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano ikiwamo Ligi Kuu Bara, baada ya kumtambulisha rasmi mshambuliaji kutoka DR Congo, Jephte Kitambala.
Katika picha iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Kitambala, ameonekana akisaini mkataba mpya mbele ya viongozi wa klabu hiyo.
Mkataba huo mpya unamfanya kuwa mchezaji wa Wanalambalamba hadi mwaka 2026, jambo linaloonyesha wazi dhamira ya klabu hiyo kujenga kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kitambala, anayejulikana kwa kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi, anatarajiwa kuongeza ushindani kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam ambayo ina ndoto ya kutwaa ubingwa msimu huu, pamoja na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Kitambala aliyezaliwa mji wa Kinshasa, amejiunga Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja, ujio wake unakwenda kuongeza ushindani katika nafasi hiyo wanayocheza Nassor Saadun aliyemaliza na mabao tisa msimu uliyopita, Abdul Suleiman ‘Sopu’ alikuwa na mabao matatu.