CP. WAKULYAMBA ASISITIZA MASHIRIKIANO BAINA YA PT NA JU


……………..

Na Sixmund Begashe, Mto wa Mbu

Jeshi la Polisi Tanzania (PT) limepongezwa kwa mashirikiano mazuri na Jeshi la Uhifadhi nchini katika kuhakikisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, misitu na malikale unakuwa endelevu kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akifunga kikao cha kihistoria baina ya Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi, chenye lengo la kubadilishana uzoefu, Mto wa Mbu Mkoani Arusha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, ameliomba Jeshi hilo kuendelea kudumisha mashirikiano na Jeshi la Uhifadhi.

Licha ya kupongeza ushirikiano huo, CP. Wakulyamba amebainisha kuwa, ushirikiano huu ni nyenzo muhimu kwa usalama wa maisha ya wananchi na mali zao, pamoja na kudumisha uhifadhi endelevu wa rasilimali za wanyamapori, misitu na malikale kwa kuwa Jeshi la Polisi linauzoefu wa miaka mingi.

“Tunaliomba Jeshi la Polisi kuendelea kutekeleza majukumu haya makubwa kwa lengo la kuendelea kulijengea uwezo Jeshi la Uhifadhi na kuimarisha ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa zilizopo katika Hifadhi zetu”. Alisema CP. Wakulyamba.

Amesisitiza kuwa ushiriki wa wajumbe wa majeshi hayo na michango waliyoitoa katika kikao hicho imethibitisha umuhimu na thamani ya ushirikiano chanya uliokuwepo na utakaoendelea kuwepo baina ya majeshi hayo.

Aidha, amewaagiza wajumbe wa kikao hicho kuzingatia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa na kujadiliwa, ikiwa ni pamoja na kusimamia na kutekeleza maazimio yaliyotokana na kikao hicho.

Pamoja na Maafisa wengine, kikao hicho kimeshirikisha, Viongozi waandamizi Wizara ya Maliasili na Utalii, Makamishana watano wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo, Makamanda wa Polisi wa Mkoa 15 nchini, Mkamanda wa Vikosi vya Polisi vitatu, wakuu wa taasisi za Jeshi la Uhifadhi, Mkamanda waandamizi wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na baadhi ya Wakuu wa Hifadhi, Mapori na Misitu Nchini.