Dar es Salaam. Benki ya CRDB imezindua CRDB Al Barakah Sukuk, hatifungani itakayokusanya fedha zitakazowezesha biashara bila riba nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.
Hatifungani hiyo, inayofuata misingi ya Kiislamu, inalenga kukusanya Sh30 bilioni na Dola milioni 5 za Marekani (Sh12.7 bilioni), huku kukiwa na uwezekano wa kuongezeka hadi kufikia Sh40 bilioni na Dola milioni 7 (Sh17.9 bilioni).
Uzinduzi huo umeifanya CRDB Al Barakah Sukuk kuwa hatifungani yenye thamani kubwa zaidi kutolewa na taasisi ya fedha nchini, na yenye ruhusa ya uwekezaji kwa sarafu zaidi ya moja.
Akizindua hatifungani hiyo mwishoni mwa wiki, Rais msaafu, Jakaya Kikwete, ameipongeza CRDB kwa kuhamasisha ujumuishaji wa wananchi wote kiuchumi.
“Hii inaleta mapinduzi katika masoko yetu ya mitaji. Inafungua fursa kwa watu waliokuwa wameachwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha kutokana na imani za kidini.
“Ni hatua kubwa ya maendeleo ya maadili na ujumuishaji wa wananchi. Nina uhakika itavutia wawekezaji wengi kuliko mnavyotarajia,” amesema Rais Kikwete.
Hii ni hatifungani ya tatu ya CRDB chini ya Mkakati wa Muda wa Kati wa 2023–2027 wenye thamani ya Dola milioni 300, uliothibitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Imefuata baada ya Green Bond na Samia Infrastructure Bond, ambazo zote zilivutia wawekezaji wengi zaidi ya matarajio.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema fedha zitakazopatikana zitaelekezwa kwenye miradi inayoendana na maadili na misingi ya Sharia, ikiwamo huduma za afya, kilimo na ufugaji, elimu, na uzalishaji rafiki wa mazingira.
“Hii inathibitisha dhamira yetu ya uwezeshaji jumuishi. Faida ni asilimia 12 kwa mwaka kwa wanaowekeza kwa shilingi, na asilimia sita kwa wanaowekeza kwa Dola za Marekani.
“Hii inalipwa kila baada ya miezi mitatu, na uwekezaji huu unaanzia Sh500,000 au Dola 1,000 (takribani Sh2.7 milioni). Dirisha litakuwa wazi hadi Septemba 12,” amesema Nsekela.
Nsekela amesema mwekezaji mkuu wa hatifungani hiyo ni British International Investment (BII) kutoka Uingereza.
Naye Balozi wa Uingereza nchini, Marianne Young, amesema uwekezaji huo utaimarisha diplomasia ya kiuchumi na ni hatifungani ya kwanza ya Kiislamu duniani kuwekewa mtaji na BII.
“Tunajivunia kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji endelevu. Sukuk hii itasaidia biashara zinazochangia ukuaji wa uchumi,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Sharia, Abdul Van Mohammed, amesisitiza kuwa ingawa hatifungani hiyo inafuata misingi ya Sharia, ipo wazi kwa kila Mtanzania aliye tayari kuwekeza.
“Tuna furaha kuwa mwekezaji mkuu wa CRDB Al Barakah Sukuk, inayoendana na misingi yetu ya uwekezaji wezeshi na kukuza upatikanaji wa mitaji barani Afrika. Sukuk inadhihirisha umuhimu wa masoko ya mitaji na dhamana katika kukuza uchumi,” amesema Mohammed.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama, na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela, wamesema uzinduzi huo ni uthibitisho wa ukuaji na uimara wa masoko ya mitaji na dhamana nchini.