KATIKA umri wa miaka 18 tu, Musa Hussein amejikuta akiwakilisha ndoto ya mamilioni ya vijana wa Afrika kwa kufunga bao katika mechi ya ufunguzi ya Sudan katika mashindano CHAN 2024.
Hussein ndiye mchezaji mdogo kabisa kufunga bao katika mashindano haya, jambo lililomfanya kuwa mchezaji wa kwanza na wa pekee aliyeweka alama akiwa na umri huo mdogo.
Alizaliwa mwezi Oktoba 2006, Hussein sio tu kuandika historia, bali pia ametangaza uwepo wake kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa kinachopaswa kufuatiliwa kwa karibu.
Katika mahojiano maalum na mtandao wa CAF, mshambuliaji huyu mdogo ameeleza furaha yake ya kutimiza ndoto ya kucheza mashindano hayo makubwa huku akitoa heshima zake kwa kocha wa Sudan, Kwesi Appiah, ambaye anamwona kama baba.
“Nimefurahi sana kushiriki katika mashindano haya makubwa. Hii ni hatua kubwa sana katika maisha yangu ya soka na ni jambo la fahari kwa mimi na familia yangu,” alisema Hussein akielezea hisia zake baada ya mechi ya ufunguzi dhidi ya Congo.
Kwa mara ya kwanza kucheza CHAN na kufunga bao ilikuwa heshima kubwa kwake. “Nashukuru sana wachezaji wenzangu kwa usaidizi wao uwanjani. Nilitamani bao letu lisirudi hadi ushindi,” aliongeza, mechi hiyo iliisha kwa sare ya bao 1-1.
Hussein ni mchezaji mdogo zaidi wa Sudan kuichezea timu hiyo katika mashindano ya CHAN, lakini tayari ameshiriki katika mechi za kufuzu CHAN pamoja na zile za Kombe la Dunia.
“Kila mara ninavalia jezi ya taifa na kujivunia sana. Ndoto yetu ni kufuzu Kombe la Dunia, ingawa ni changamoto, hatutakata tamaa,” alisema.
Marafiki zake kutoka Mji wa Kassala walimpa jina la utani Kante.