Wanariadha chipukizi Fabian Sulle na Noella Peter kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani wameng’ara vema katika mbio za Clock Tower Half Marathon zilizomalizika jijini Arusha leo Agosti 10, 2025.
Wanariadha hao mbali na kuibuka na ushindi pia wamevunja pia rekodi zao binafsi za muda wa umbali wa kilomita 21 katika mbio hizo zilizoanzia mzunguko wa Clock Tower na kuishia viwanja vya Gymkhana.
Fabian Sulle kutoka klabu ya Polisi Tanzania aliyekuwa na muda bora wa saa 1:07, leo ameivunja baada ya kutumia saa 1:05:23 kumaliza mbio hizo akifuatiwa na Protas Gabriel aliyemaliza kwa saa 1;05:44 na Nestory Stephen kwa saa 1:06:41 wote kutoka Singida.
Kwa upande wa wanawake Noella Peter kutoka klabu ya JKT aliyekuwa na muda bora 1:19, leo ameweka rekodi mpya ya kumaliza mbio hizo kwa saa 1:17:01, akifuatiwa na Catherine Lange kutoka Magereza aliyetumia saa 1:17:43 na Banuela Katesyinga kutoka Klabu ya Moshi kwa saa 1:34:35.
Katika mbio hizo zilizokimbiwa pia kilomita 10, wanaume Michael Leonada alikata upepo kwa dakika 31:32 akifuatiwa na Shomari Mohamed aliyefuatia kwa dakika 31:36 wote kutoka klabu ya Talent klabu na nafasi ya tatu alimaliza Nicodemas Joseph kwa dakika 31:50.
Naomi Kidumbanda alishinda mbio hizo kwa wanawake akitumia dakika 38:15 akifuatiwa na Deborah Benedict kutoka JWTZ aliyemaliza kwa dakika 39:05 na Joyce Damian wa Arusha aliyetumia dakika 40:24.
Akizungumzia ushindi huo, Fabian amesema alitamani kuona jinsi anavyopunguza muda wake katika mbio za kilomita 21 ikiwa ni sehemu ya mazoezi kuelekea mbio za Dunia za Nyika zinazotarajiwa kufanyika Januari 2026, Marekani.
“Namshukuru Mungu kwa ushindi huu na nimeona nafasi yangu na nitazidi kufanya mazoezi kuhakikisha naiwakilisha nchi yangu vema katika mashindano makubwa ya dunia yaliyoko mbele yetu,” amesema.
Mwenyekiti wa klabu ya Arusha Runners awalioandaa mbio hizo Issack Shayo, amesema zaidi ya wanariadha 1000 wameshiriki mbio hizo zenye lengo la kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, lakini upandaji wa miti kwa ajili ya kutunza mazingira.
“Tunatamani taifa lenye afya njema na uchumi ulioendelea, lakini bila hamasa ya mazoezi tutaendelea kutumia gharama kubwa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kushusha nguvu kazi ya kuingiza kipato, ndio maana Arusha Runners tuko hapa kuhakikisha tunawavuta watu kufanya mazoezi na baadae tutapanda miti kwenye maeneo ya umma,” amesema.
Mdhamini mkuu wa mbio hizo, kutoka kampuni ya kitalii ya Solo Adventure, Athumani Njiku amesema udhamini wao umelenga kufanikisha malengo makubwa ya mbio hizo ikiwemo uboreshaji wa afya na utunzaji wa mazingira.
“Lakini kuita mbio hizi katika mnara wetu wa Clock Tower unatumika kutangaza pia utalii wetu ambao ni kitovu cha uchumi wa Mkoa wa Arusha,” amesema.
Afisa Michezo Jiji la Arusha, Benson Maneno amewataka wakazi wa Arusha na viunga vyake kuwa na desturi ya kuhudhuria mbio na tamasha za mazoezi kila zinazojitokeza ili kukabiliana na vifo vya ghafla lakini pia maradhi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA), Rogath John Stephen amesema mbio hizo zimekuwa chachu kubwa ya kuhamasisha wanariadha chipukizi kuonyesha uwezo wao hivyo kuwarahisishia kibarua cha kusaka timu za kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.
“Mfano leo umeona Fabiana na Noella wamezidi kuweka rekodi ya muda wao bora, hii ni ishara kwamba wanapambana kwenye mazoezi hivyo watakuwa kipaumbele kwenye maandalizi ya timu yetu ya Taifa kuelekea michuano ya Nyika Januari 2026, yatakayofanyika Marekani.”