Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Hayati Job Yustino Ndugai alikuwa kiongozi mkomavu kisiasa na kiuongozi, ambaye aliweka thamani kubwa katika demokrasia ya Bunge.
“Hayati Ndugai alikuwa mkomavu kisiasa na kiuongozi, na aliyeamini katika demokrasia ya Bunge. Alipokuwa Spika, Bunge lilishuhudia mafanikio mbalimbali yaliyoelezwa hapa na Katibu wa Bunge lakini pia Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliyasema hayo tarehe 10 Agosti 2025, katika viunga vya Bunge jijini Dodoma, wakati wa hafla ya kuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ndugai, aliyefariki dunia hivi karibuni. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wabunge, ndugu, jamaa na wananchi waliojitokeza kumuenzi marehemu.